M
|
WENYEKITI wa Taasisi ya Tanzania Mzalendo
Foundation,Khamis Mgeja,amepongeza jitihada za Rais ,John Pombe Magufuli,kupambana
dhidi ya ubadhirifu
wa Rasilimali za nchi,na kudai vitendo hivyo ni matokeo ya Mfumo
ndani ya Serikali ya Chama Cha Mapinduzi.
Mfumo umesababisha baadhi ya Watumishi
Serikalini,kutenda ubadhirifu huo, huku akidai utaratibu unaotumika
kuwawajibisha hauna tija kwa Watanzania.
Kauli hiyo aliitoa jana mjini
Kahama,akiwa mapumzikoni nyumbani kwake mtaa wa Nyasubi Mjini
Kahama,alipotembelewa na kuongea na baadhi ya wazee maarufu wa itikadi na
kada mbalimbali za Kisiasa,ambao waliongozwa na Mzee Jozia Kazi Ngwanateleza
kutoka Kata ya Malunga,wilayani Kahama.
Wazee hao walitaka kujua hali ya sasa
ya nchi inavyoendelea kisiasa,kiuchumi pamoja na masuala ya demokrasia
yanayofanywa na serikali ya awamu ya Tano,na kusimamiwa na Rais John Pombe
Magufuli.
Mgeja akizungumza na Wazee hao
aliwaambia wakati umefika ni vizuri kufanya tathimini ya kina kwa kazi
zinazofanywa na Serikali ya CCM awamu ya tano kwa ujumla ikisimamiwa na Rais
John Pombe Magufuli,inaonesha dhamira ya dhati kutaka rasilimali za Taifa
zinufaishe umma.
Katika mazungumzo hayo Mgeja alisema
pamoja na Rais Magufuli,amekuwa akisema mara kwa mara kuwa nchi hii imeibiwa
sana, hasa katika maeneo ya Bandari,Makinikia ya
Dhahabu,Almasi,Tanzanite,mishahara hewa na wafanyakazi hewa,alidai hayo ni
matunda yanayotokana na mfumo mbovu uliopo na kusimamiwa na Serikali ya CCM.
Alisema pamoja na kwamba kila tatizo
la wizi na upotevu wa mali za umma linapotokea imekuwa kasumba ya Mawaziri
kujiuzuru jambo ambalo Watanzania hawanufaiki nalo hata kwa kijiko cha
sukari,kwa kujiuzuru kwao,hivyo hatua zaidi zilipaswa kufanyika ili kuleta tija
kwa Taifa.
“ Ni vyema Watanzania wakati umefika
tuambizane ukweli,kinachosababisha mianya ya wizi na ubadhirifu wa rasilimali
za nchi,ni mfumo uliojengwa ukatungiwa sheria,ukasimamiwa na Watawala wa
Serikali ya Chama cha Mapinduzi za awamu zote zilizopita za pili,tatu na nne na
iliyopo sasa ya awamu ya tano,”alisema Mgeja.
Aliendelea kusema kitendo cha Mawaziri
wa Wizara husika kujiuzuru mara kwa mara ni sawa sawa na kuwatoa kafara na
kudai haingii akilini na haiwezekani Waziri kuamua jambo bila Baraza la
Mawaziri ama Rais kujua.
Alisema Nchi nyingi Duniani zimepata
anguko la Kiutawala kutoka Chama kilichopo madarakani ambacho kimepewa dhamana
ya kuongoza nchi na kulinda rasilimali na kupelekea kupata kashfa nzito juu ya
wizi na ubadhirifu wa rasilimali za nchi.
Kwa upande wao Wazee hao,walishauri
kama nchi hapa tulipofika tusitafute mchawi wala kuendelea kuchimbua
makaburi,hakuna atakayebaki salama tatizo kubwa la nchi yetu iliyopelekea
kuibiwa ni sababu ya mfumo ulioasisiwa na Serikali ya CCM.
Wazee hao walimuomba Rais
Magufuli,masuala mawili muhimu kwa manufaa ya Taifa,ambayo ni Suala la
kukamilisha Mchakato wa Katiba mpya,pili aelekeze kuangalia ubadhirifu katika
maeneo mengine haswa masuala ya gesi,maliasili na upande wa miundo mbinu ambapo
kuna barabara nyingi zimejengwa chini ya kiwango na tayari zimegharimu
mabilioni ya Shilingi.
Walisisitiza juu ya upatikanaji wa katiba
mpya kwakuwa itakuwa muongozo mkubwa na muarobaini katika kutekeleza
demokrasia,masuala ya kiuchumi na siasa.