Wednesday, August 21, 2013

UTANDAWAZI UMEATHIRI MILA ZETU WATANZANIA

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO

Nchini Tanzania kuna makabila mengi ambapo baina yake,kuna utani wa jadi miongoni mwao.Utani huu wa jadi upo karne na karne kabla hata nchi yetu haijawa chini ya utawala wa kikoloni,na sijui ulitokea wapi?Na kabila ambalo linaloongoza kuwa na watani wengi kutoka maeneo karibu yote nchini,ni kabila la Wasukuma na wenzao Wanyamwezi.
Zama hizo hadi kufikia mwanzoni wa uhuru wa Taifa letu utani wa jadi ulikuwa na nguvu.Kila mmoja alimdhihaki na kumkejeli ama kumsema hata kumcheka mtani wake mbele ya kadamnasi,kulikuwapo na vituko na majigambo yaliyofanyika ama katika ngoma za jadi na kwenye vilabu vya pombe za asili ambayo yalileta burudani ya aina yake.
Lakini utani huo wa jadi katika karne tulionayo,umekuwa hasi tofauti na zama za mababu na bibi zetu,sababu kubwa ikiwa ni  mabadiriko ya sayansi na teknolojia.Utandawazi  umekuwa athari kubwa kwa Jamii ya Watanzania kubeba asili yetu na kutawaliwa na tamaduni za kutoka nchi za Magharibi.
Zama hizo za karne ya kumi na Tisa kurejea nyuma,Makabila ya Watanzania yalithamini utamaduni huo wa kimila ambao uliwafanya watu kuambiana ama kutendeana jambo lolote katika kipindi cha furaha na majonzi pasipo chuki.Masihara yaliofanyika yalidumisha Mila na desturi ya kila kabila la Muhusika.
Nyakati zingine;Dhihaka hizo ziliambatana na faini,hidaya na hata mchango kulingana na Nasaba moja hadi nyingine,kuwa na tukio la burudani ama huzuni,au katika mfumo wa maisha ya kila siku,Mmoja kujisahau na kutenda jambo litakalotoa faida ya hidaya kwa watani zake.
Mzee  wa kabila la Kingoni;Andrew Chitete {75}mkazi wa kitongoji cha Kasela Kata ya Malunga wilayani Kahama,ameonekana kutoathirika na Utandawazi uliopo kutokana na mfumo wake wa Maisha kuhakikisha anaendeleza mila na desturi hizo za Mababu na Mabibi,kwa kinywa chake kutawaliwa na maneno ya utani usioleta Ufidhuli kwa mtu wa Jinsi na umri wowote ilimradi akijilidhisha ni mtani wake.Japo dhihaki zake kuna kipindi zilitaka kumletea athari.
Amekuwa akijitokeza kufanya utani katika hadhara mbalimbali  na kuleta burudani ya aina yake na kipindi kingine kufanya tukio la kuogofya ,ambapo matukio hayo mara nyingi amekuwa akiyafanya misibani .Kama kutumbukia  kaburini na kukumbatia sanduku la marehemu mtani wake lisifukiwe kukamilisha maziko hadi pale watani wake wanapompatia  fedha ndipo huruhusu kukamilisha maziko hayo.Ufyosi wa namna hii haufanyiki  maeneo mengi nchini na haujapata kutokea karibu robo karne sasa.
Mzee Chitete hufanya utani  kwa watu ambao amejiridhisha kuwa ni watani zake wa jadi,huku lengo la ufyosi wake  ni kudumisha Mila na asili ya Mtanzania.
Anasema; “Ni vyema tukumbuke utani wetu wa jadi,ambao wazee wetu wa zamani walikuwa wakiutenda pasipo kupotosha ambapo katika misiba ilisaidia kupunguza machungu ya wafiwa.Na utani kama huu nimeufanya mara nyingi hata kwenye maziko ya mama yake na Jaji Ihema yaliyofanyika Kata ya Isagehe wilayani Kahama,nilitwaa Mishumaa yote na kuzuia maiti isizikwe katika kaburi lililoandaliwa na kudai nataka kuusafirisha mwili wa marehemu kuupeleka kwetu Songea kuuzika,nilipochangiwa fedha niliruhusu maiti kuzikwa.”.
“ Utani unatambulika Kisheria ndio maana katika Maziko ya mzazi wa Jaji Ihema ilipotaka kutokea vurugu kwa baadhi ya watu wasioelewa utani kutaka kunishushia kipigo,Jaji aliwazuia kwa kuwaeleza kuwa nina haki,huku akiwa miongoni mwa waliochanga pesa ili niruhusu maiti izikwe,”Alisema Mzee Chitete.
Alikanusha kuitumia misiba ya makabila ya Watani wake kama ni miongoni mwa mradi wa kumuingizia kipato kwa kubainisha kuwa pesa anazochangiwa pindi anapozuia maziko huzitumia kununua bidhaa mbalimbali kama Mchele,Unga,Chumvi,Sukari,Dagaa,Maharagwe na vinginevyo ambavyo huvipeleka kuwapa pole Wafiwa.
Mzee Chitete alisema ni ada yake kufanya ufyosi kwa Mtani wake katika mazingira yoyote yale,wakati wa raha,wa kawaida na vipindi vya misiba na kukisisitizia kizazi kilichopo kuuenzi Utamaduni wa makabila yetu kwa kutokuwa watumwa wa fikra kwa kuthamini Mila na Desturi za Ughaibuni na Ulaya.
Tumo katika kifungo cha fikra, ndio maana maadili kwa vijana wa leo ni ruya,Utumwa wa Utandawazi ni anguko la asili yetu kwa kubeza UTANI WA JADI,ambao ulikuwa silaha hata ya kurekebisha Vijana walio kuwa katika dalili za kupotea kwa kuwarejesha katika Mstari wa tabia njema,tofauti na leo ambapo Vijana si ajabu kupita nusu Uchi hata kwa wakwe zao sembuse wazazi wake?
Kwa mwenendo uliopo na kasi ya utandawazi unazidi kuathiri mila zetu BURIANI  UTANI WA JADI TANZANIA.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI