Thursday, September 9, 2010

MADHARA YA MATUMIZI YA MUDA MREFU WA MADAWA YA MAJIRA

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO

PAMOJA na Serikali kuwa na sera ya uzazi wa mpango na kuridhia matumizi ya vidonge au sindano za majira ama njia za njiti ili kuzuia kupata mimba huku ikidhibiti kwa kuwafungulia mashitaka wanaojitokeza kupinga hadharani matumizi hayo,lakini ni dhahiri matumizi ya muda mrefu huwaletea madhara.

Miongoni mwa akina mama waliokumbwa na madhara ya matumizi hayo ya dawa za majira ni Easter Katuga ( 58 )mkazi wa Kijiji cha Igunda wilayani Kahama ambaye ililazimika kufanyiwa Opresheni ili kunusuru uhai wake baada ya kukabiliwa na uvimbe tumboni unaosadikiwa kusababishwa na matumizi ya madawa ya majira.

Bi Easter alifanyiwa upasuaji huo Agosti 19 mwaka huu katika hospitali binafsi ya Igalilimi iliyopo mjini Kahama baada ya kukaa na uvimbe huo uliomsumbua kiasi cha kuonekana kama mjamzito kwa kipindi cha miaka mitano.

Akielezea madhira hayo yaliyomsibu bi Katuga alisema kuwa baada ya kuolewa na kuzalishwa watoto watatu mfululizo,shoga zake walimshauri kutumia dawa za majira ili kuepuka kuuchosha mwili kiasi cha kuzeeka haraka kutokana na kuzaa mfululizo.

Aliendelea kueleza kuwa matumizi ya dawa za majira hakumshirikisha mmewe kwa kuhofia kutokea marumbano ambayo yangehatarisha ndoa yake.

Hata hivyo alisema baada ya kupita miaka mingi aliacha matumizi ya dawa hizo kusudi apate mimba lakini haikutokea hadi kulazimika kutumia dawa za jadi ili kusogeza kizazi.

Alibainisha kwamba baada ya kuacha matumizi ya dawa hizo ili kukidhi matakwa yake ya kuzaa kwa mpango na huku akiwa ametumia dawa za kienyeji za kumuwezesha kunasa mimba,alijaaliwa kubebeshwa mimba tatu ambazo zote ziliharibika kabla ya kupata uvimbe aliodhani awali kuwa ni mimba.

Akizungumzia juu ya kuwepo kwa madhara ya dawa za uzazi wa mpango,Daktari mmoja ambaye hakupenda jina lake litajwe kwakuhofia kupoteza kazi hasa kwakuwa Serikali inasisitiza uzazi wa mpango wa kutumia dawa za majira,alikiri kuwepo kwa madhara ya matumizi ya dawa za majira.

Daktari huyo alifafanua kuwa matumizi ya muda mrefu wa dawa hizo husababisha madhara ya uvimbe tumboni sambamba na kuwepo kwa mabadiliko mengi mwilini kwa mwanamke na hata sehemu za siri.

Akifafanua zaidi alisema madawa hayo pia huharibu mfumo wa hedhi na nyumba ya uzazi kiasi cha kuchelewa ama kutoweza kupata mimba kabisa kutokana na kuathiri homoni zinazochochea uzazi,na wengine hupatwa pia na fungasi sehemu za siri na maradhi mengine yanayoweza kushambulia sehemu hizo kama vile kutoka maji machafu yenye harufu mbaya.

Aidha alitumia fursa hii kuiasa jamii kutokurupuka katika matumizi ya vidonge vya majira pasipo ushauri wa daktari,ili kuepukana na madhara kama hayo yanayoweza kuwapata ambayo yatawaathiri kisaikolojia na kuathiri mfumo mzima wa maisha ya akina mama watakaokumbwa na madhara hayo.

MWISHO.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI