MGODI wa dhahabu wa
Bulyanhulu,unaomilikiwa na Kampuni ya Acacia,umetakiwa kudumisha mahusiano na
majirani wanaozunguka uwekezaji wake,na kuhakikisha unakuwa mstari wa mbele
kuchangia miradi
inayoibuliwa na wananchi.
Aidha umetakiwa kubaini na kuondoa
kero zinazowakabili wananchi wa wanaoishi kumzunguka mwekezaji huyo,hatua
itakayozidi kuchangia kuwepo kwa maendeleo ya miradi ya wananchi,itakayokuza
uchumi,na kuondokana na migogoro kama inayotokea maeneo mengine ya wawekezaji
nchini.
Mkuu wa Wilaya ya Nyang’wale mkoani
Geita, Hamimu Gwiyama,anapongeza mahusiano mazuri yaliyopo baina ya Mgodi wa
Bulyanhulu na vijiji vinavyouzunguka.
Anasema ameridhishwa na mahusiano
makubwa aliyoyakuta kwenye Wilaya jirani ya Kahama Mkoani Shinyanga na
wawekezaji wa mgodi wa Bulyanhulu kwa madai yamechangia kuwepo kwa maendeleo,katika
eneo husika.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya
ya Kahama Fadhil Nkurlu,katika uwanja wa shule ya msingi Kakola Kata ya
Bulyanhulu Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama,Gwayima aliupongeza mgodi kwa
kudumisha mahusiano ambayo yamekuwa chachu ya maendeleo kwa wananchi.
Alisema kuna maeneo nchini kuna
migogoro baina ya wawekezaji na wananchi,na kudai wakati umefika kwa wawekezaji
na wananchi kwa pamoja kuwa na mahusianao mazuri ili kuweza kuwa na uwekezaji
wenye tija kwa pande zote mbili kwa kuharakisha maendeleo ya nchi.
“Mashirikiano haya mazuri
naomba myadumishe kwani Mgodi utapokuwa na mahusiano mazuri na wananchi
wanaozunguka maeneo yake, kutasaidia utekelezaji mzuri wa miradi mbalimbali ya
maendeleo kwa wakazi,wanaoishi katika vijiji 14 vinavyozunguka
mgodi.”Alisema Mkuu huyo wa wilaya.
Aidha Gwiyama alisema pasipo
mahusiano mazuri mgodi hautaweza kutekeleza shughuli za maendeleo kwa wakazi
hao, ambao ni jirani zao, badala yake itatawala migongano isiyokuwa na
tija baina ya wakazi hao na uongozi wa mgodi.
“Ni wapongeze kwa kitendo cha
uongozi wa Acacia kubuni mbinu ya kunyanyua vipaji vya michezo mbalimbali
sehemu anayowekeza ni jambo jema,hali hii inaonyesha wazi wanania ya dhati ya
kuwasogeza karibu Wananchi waliopo sehemu wanayowekeza” alisema Gwiyama.
Aliongeza kwa kusema,“Niwaase
uongozi wa mgodi huu,msiishie kudhamini leo tu,tafadhari endeleeni kufadhili
michezo mbalimbali kwa Wananchi wa halmashauri ya Msalala na ibueni vipaji
hivyo ili tupate wachezaji wa kimataifa kutoka Msalala na pia mshirikishe na
washiriki kutoka Wilaya yangu ya Nyang’hwale
Kwa upande wake Meneja
Mahusiano ya jamii wa Acacia Bulyanhulu, Sara Terry, alisema lengo
la Mgodi ni kudumisha mahusiano baina ya Wananchi na mgodi huo,ndio sababu ya
kufadhili bonanza hilo,hali itakayodumusha amani na kuufanya mgodi kutekeleza
shughuli za maendeleo kwa wananchi pamoja na kufanya shughuli za uwekezaji ziwe
za ufanisi zaidi.
Bonanza hilo liliandaliwa na shirika
lisilo la kiserikali la Search for Common Ground linalofanya shughuli zake
ndani ya mgodi wa Bulyanhulu ambapo hilo limefadhiliwa na kampuni ya Acacia
ambapo mratibu wa Thomas Magesa alisema lengo lake ni kuimalisha mahusiano
kutokana na shirika lake kujihusisha na maswala ya usuluhisho wa migogoro.