MGODI wa Dhahabu wa
Bulyanhulu,wilayani Kahama,unaomilikiwa na Kampuni ya ACACIA,umekabidhi
madawati 2000 yenye thamani ya Shilingi 240,800,000/- yatakayogawiwa katika
Shule za Msingi na Sekondari mkoani Shinyanga.
Akizungumza katika hafla fupi
ya kukabidhi madawati hayo,iliyofanyika uwanja wa michezo wa Halmashauri ya Mji
wa Kahama,Afisa Ufanisi na Ustawi wa Mgodi wa Bulyanhulu,Elias Kasitila,
alisema hiyo ni awamu ya nne kukabidhi madawati kwa kipindi cha mwaka 2016,ili
kutekeleza kampeni ya serikali
kuhakikisha kila mwanafunzi anaketi kwenye dawati.
Kasitila alisema mbali ya mgodi huo kukabidhi dawati kwa awamu nne
tofauti,umekuwa mstari wa mbele kukichangia
sekta ya elimu Wilaya za Kahama,mkoani Shinyanga na Nyangh’wale mkoani
Geita, ikiwemo nyumba za walimu, Maabara, vyumba vya madarasa na vifaa vya taaluma.
“Tumekuwa tukishirikiana na
jamii kutekeleza miradi mbalimbali ya elimu pia mgodi unadhamini masomo kwa
wanafunzi,yote hayo lengo likiwa ni kuboresha mazingira ya elimu nchini
Tanzania,”alisema Kasitila.
Akipokea madawati hayo kutoka
Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack,alidai
mkoa wake bado unakabiliwa na changamoto kadhaa za kielimu ambazo zimekuwa
kichocheo cha kushuka kwa kiwango cha taaluma,zikiwemo kukosekana kwa Nyumba za
Walimu na Mabweni ya wanafunzi.
Telack alisema Wilaya za
Kahama na Kishapu, bado zinakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa nyumba za
walimu na mabweni ya wanafunzi kwa shule za sekondari,na kusababisha walimu na
wanafunzi kutembea umbali mrefu,kufika shuleni kiasi cha kupunguza ari ya
ufundishaji na upokeaji mafunzo.
“....kuna shule za Msingi katika wilaya hizi,hazina
nyumba za walimu,na kuwalazimu walimu kusafiri kila siku kilometa 8 kwenda na
kurudi kazini, hali ambayo huwafanya kufika shuleni wamechoka na ufanisi wa
kufanya kazi ipasavyo hupungua,”alisema Telack.
Aidha Mkuu wa Mkoa huyo alisema katika Wilaya hizo zipo shule za
sekondari za Kata,zilizojengwa mbali na makazi,na kulazimu wanafunzi kukimbia
kuwahi masomo kwa kusafiri umbali wa kilometa 16 kwenda na kurudi,ambapo hufika
wamechoka na kutopokea vizuri masomo wafundishwayo.
Hivyo mkuu huyo wa Mkoa
aliwaomba viongozi wa migodi yote ya Bulyanhulu na Buzwagi pamoja na ule wa
Almasi uliopo Mkoani Shinyanga kuweka nguvu zaidi kuchangia sekta ya elimu Wilayani Kahama kwenye shule ambayo haina
nyumba za walimu, na Wilayani Kishapu kwenye sekondari isiyokuwa na
mabweni.