MATUKIO ya mauaji ya vikongwe kwa
imani za kishirikina,yameanza kurejea kwa kasi wilayani Kahama,ambapo kwa mwaka
huu,vikongwe saba vimeuawa kutokana na imani potofu inayochangiwa na jamii
kukosa elimu ya afya inayochangia vifo vya uzembe wa kutowahi matibabu mapema.
Akiongea kwa niaba ya Mkuu wa wilaya
ya Kahama,Katibu Tawala wa wilaya ya Kahama, Thimothy Ndanya,alibainisha
kwamba katika kipindi cha January hadi Agosti mwaka huu tayari matukio
sita ya vikongwe kuuawa kwa imani za kishirikina yametokea,kiwango ambacho
amedai ni kikubwa mno kupata kutokea katika wilaya ya Kahama.
Ndanya aliyataja maeneo katika
wilaya ya Kahama,ambayo yamekuwa yakitokea matukio hayo ya mauaji mara kwa mara
kuwa ni Kata za Kilago katika Halmashauri ya Mji wa Kahama, Chambo na Idahina
katika Halmashauri ya Ushetu,huku matukio mawili yaliyosababisa vifo vya watu
watatu yakitokea katika Kata mmoja ya Chambo.
Aidha alisema katika tukio
lililotokea Agosti 9,mwaka huu la kuuwawa Vikongwe viwili katika Kata ya
Chambo,limeshangaza kuona viongozi wanaopewa dhamana ya kuongoza umma nao
kuendelea kutawaliwa na fikra za ushirikina,kutokana na muhusika mkuu
kuwa kiongozi wa serikali ya Kijiji.
“….imeshangaza kuona mwenyekiti wa
kijiji hicho ambaye amekimbia na familia yake,kutokuwa kioo cha jamii,kuongoza
uhalifu kwa kuwachoma moto vikongwe hao,huku taarifa ya daktari ikionesha
mwanae kufariki kwa kutokwa na damu baada ya kujifungua,lakini yeye kuamini
vikongwe wale walimroga binti yake,kwakweli suala hili serikali haitalifumbia
macho kwani haiko tayari kushuhudia wananchi wake wakiuuawa.”Alisema Ndanya.
Aliikumbusha jamii hasa ya vijijini
kuwa na utaratibu wa kupima afya zao mara kwa mara huku ikianzisha mazoea ya
kukimbilia katika zahanati ama vituo vya afya pindi wanapougua,kuliko kuchelewa
katika matibabu ambayo gharama yake huwa ni vifo ambavyo huwaingiza katika
imani za kishirikina.
Kufuatia vifo hivyo vya vikongwe
hivyo vilivyofahamika kwa jina moja moja la Mwanabunzali na Mwanazwazwa,Mkuu wa
wilaya ya Kahama, Fadhili Nkurlu,ametangaza msako mkali dhidi ya Mwenyekiti wa
Kijiji cha Chambo,Clement Shija, pamoja na wenzake waliohusika kuuwa vikongwe
hao.
Jeshi la Polisi mkoa wa Shinyanga,linaendelea
na uchunguzi juu ya tukio hilo la mauaji kwa kuwashikilia watu kadhaa
katika Kata hiyo ya Chambo,na jitihada zikiendelea za kuwapata wahusika wengine
wakiongozwa na Mwenyekiti huyo ambao wamezikimbia familia zao.