KATIKA kuhakikisha mkulima
hapunjwi katika mauzo ya mazao yake,Serikali Kata ya Isaka imepiga marufuku
Wafanyabiashara kutoka maeneo mbalimbali nchini kufika eneo hilo wakiwa na
vipimo visvyo stahili vinavyomnyanyasa Mkulima.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa
Mtendaji Kata ya Isaka,Mwanaidi Mustafa Mzee,katika mikutano ya hadhara
iliyoitishwa na Diwani wa Kata hiyo;Gerald Mwanzia,ambapo alisema atahakikisha
anawachukulia hatua kali za kisheria Wafanyabiashara watakaofika na kumpunja
Mkulima.
Afisa Mtendaji huyo
aliwaomba wakulima kutokubali kuendelea kunyanyasika kwa kuendekeza shida
zao,bali wahakikishe wanauza ziada ya mazao yao kwa faida kwa kutumia vipimo
sahihi vinavykubalika.
“Kwakuwa ni kawaida
kutumia vipimo vya asili,kama ndoo za plastiki,basi ni marufuku mfanyabiashara
kuja ndoo yake bali wazikute kwenu ambazo mmeridhia kuwa haziwapunji,msikubali
kutumia ndoo zao maarufu kwa jina la Msumbiji zinakupunjeni na kumpa faida
kubwa zaidi Mfanyabiashara,”alisema Afisa Mtendaji huyo.
Kwa upande wake Diwani wa
Kata ya Isaka,Mwanzia,alisema Kamati ya Maendeleo ya Kata yake imeanza mkakati
wa maendeleo kwa kutafiti changamoto katika sekta za Elimu na Afya,huku
wakianzisha mfuko wa kuendeleza sekta hizo.
Mwanzia alisema wanahitaji
kuboresha sekta hizo ziwe na tija kwa Kata hiyo hivyo ni budi wananchi
washikamane na Kamati ya Maendeleo kwa kuchangia mfuko huo,ambao utaanza
kujikita zaidi katika kuboresha miundo mbinu katika sekta za Afya na Elimu.
“Tusihadaike na kufaulu
Elimu Bure pasipo kufanya jitihada za kuboresha miundo mbinu yake kama majengo
ya madarasa,ambayo bado mwananchi nguvu zake zinahitajika na si kutegemea
serikali pekee,”alisema Mwanzia.