VIONGOZI wa dini
wamesisitizwa kuzidi kuliombea Taifa sambamba na wananchi ili wajenge mioyo ya
kizalendo iliyopandikizwa na waasisi wa taifa hili,kwa kujitoa kuchangia
shughuli za Maendeleo katika maeneo wanayoishi.
Diwani wa Kata ya
Isaka,Gerald Mwanzia,aliyasema hayo katika uzinduzi wa Kwaya ya Mtakatifu
Fransisco wa Sale ya Dhehebu la Romani Katoliki,Parokia ya Isaka,ambapo alisema
jamii wamekuwa wagumu kuchangia shughuli za maendeleo,hivyo kustahili kuombewa.
Alisema Viongozi wa Dini
wanastahili kuunga jitihada za Rais wa Awamu ya tano,John Magufuli,kwa
kumuombea aendelee na jitihada alizozianzisha za kutetea maslahi ya
umma,sambamba na kuiombea jamii kuwa na moyo wa kizalendo na kujitoa kuchangia
maendeleo ya nchi.
“Viongozi wa dini
mnawajibu mkubwa kuomba na kuwaongoza waumini wenu kwa kuwajenga katika imani
za kizalendo,na hili litekelezeni hata kwa kupitia kuwezesha vikundi vya Kwaya
kutoa ujumbe kupitia nyimbo zao,”alisema Mwanzia.
Aliongeza kusema, “…ili
Taifa lifanye vyema linahitaji kuombewa,na kwakuwa wananchi nao wagumu
kuchangia maendeleo kwa kunung’unika pindi watakiwapo kuchangia shughuli za
maendeleo,huku wakitaraji maendeleo ambayo kwa yakini watajiletea wenyewe,nao
waombewe.”
Kwa upande wake Paroko wa
Kanisa la Isaka,Peter Kadundu,aliasa jamii kuwa na moyo wa upendo,kuvumiliana
na kusameheana huku ikizingatia kulijenga Taifa kwa kuzingatia maadili mema.
Akisoma
risala,mwanakwaya,Michael Emmanuel,alisema albamu yao hiyo iitwayo,Yatafakari
Matendo yako,ni ya kwanza kutoa ikiwa na nyimbo tisa,ambapo mauzo yake
wanatarajia kuyatumia kununua kinanda na vifaa kadhaa vya kanisa kwa lengo la
kuendeshea Ibada.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI