WATU saba wa familia moja katika wilaya ya Sengerema,mkoani Mwanza,wameuawa kikatili,kwa kuchinjwa na watu wasiofahamika walipokuwa wamelala nyumbani kwao.
Mauaji hayo yalitokea saa nane usiku wa kuamkia jana,katika kijiji cha Sima wilayani humo,huku watu wanne wa familia hiyo wakinusurika kifo.
Taarifa
iliyotolewa na Ofisa Habari wa Mkoa wa Mwanza, Atley Kuni ambaye
alifuatana na Mkuu wa Mkoa huo, John Mongella na Kamanda wa Polisi Mkoa,
Ahmed Msangi katika eneo la tukio, alisema watuhumiwa katika tukio hilo
hawajajulikana.
Kuni
aliwataja waliopoteza maisha katika tukio hilo kuwa ni Augenia Philipo
(62), Maria Philipo (56), Yohana Mabula (20), Regina Aloyce (12) na
Mkiwa Philipo (13) huku wengine wawili wakitambulika kwa jina moja kila
mmoja kuwa ni Donald na Samson.
Aidha,
chanzo cha mauaji hayo ya kikatili hakijajulikana, ingawa Mkuu wa
Wilaya ya Sengerema, Zainab Telack alisema huenda mauaji hayo
inawezekana yakawa ni ya kulipiza kisasi.
Vyanzo
vingine vinaarifu kuwa mauaji ya namna hiyo ni ya kawaida katika maeneo
hayo, hasa msimu huu ambao kaya nyingi zinakaribia msimu wa mavuno.
“Bado
kuna mkanganyiko juu ya chanzo cha mauaji hayo, wapo wanaosema kuwa
huenda ni ya kulipiza kisasi lakini pia wengine wanasema yanatokana na
msimu wa mavuno, lakini tunaamini uchunguzi wa Polisi ndio utakuja na
majibu sahihi na ambao umeshaanza kazi hivi tunavyoongea,” alisema Kuni.
Baadhi ya majirani wa familia hiyo walidai mauaji hayo yanaweza kuwa yamechochewa na uhasama wa mashamba,huku baadhi yao kutokana na kutokea mauaji hayo wameanza kuzikimbia familia zao,wakihofia kukamatwa kusaidia upelelezi.
Hata hivyo walidai tukio la namna hiyo ambalo pia linahusishwa na kisasi,halijawahi kutokea wilayani humo,hivyo baadhi yao kuingiwa na hofu ya kukumbana na mkono wa dola pasipo kuhusika na tukio hilo.