MKUU wa Mkoa wa Dar es
Salaam ameamuru vyombo vya dola kuchunguza kontena 115 ya sukari
iliyokuwa inasafirishwa kwenda nchini Uganda.
Sukari hiyo ilikuwa imehifadhiwa kwenye Bandari Kavu (ICD) moja iliyopo Barabara ya Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Agizo hilo lilitolewa
Dar es Salaam jana baada Makonda akiwa ameongozana na Mkuu wa Wilaya ya
Ilala Raymond Mushi na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Sophia Mjema baada
kufanya ukaguzi katika bandari Kavu na baadhi ya maghala ya kuhifadhi
nafaka.
Akizungumza jana Makonda alishangazwa kuona kontena hizo 115 ambazo zilikuwa njiani kusafirishwa nchini Uganda.
"Naambiwa sukari hii
iko katika makontena 115, lakini vyanzo vyangu mimi vinaonesha kuwa hapa
kuna makontena ya sukari 164, lakini sisi tumetembelea ghala hili
wametuambia kuwa wana eneo lao la kuwekeza mizigo yao, lakini si huku
sasa inakuwaje tena makontena haya yaletwe huku tena... yamechanganywa
ili yasionekane sasa naamuru uchunguzi ufanyike mara moja,"alisema
Makonda.
Makonda alisema ni
lazima Watanzania wajue kuwa kazi hii inapofanyika hakuna kuweka suala
la uchama, kwani maendeleo yanahitajika kwa kila mtu aliye ndani ya
chama chake.
Alisema ameambiwa
sukari hiyo ilikuwa inasafirishwa kupelekwa nchini Uganda, lakini
wameamua kubadilisha kibali kwa kuwa nchini kuna tatizo la sukari.
Hata hivyo alisema
hakubaliani nalo kabisa kwani huo ndiyo mchezo wa wafanyabiashara
kukwepa kodi kwa kuingiza mzigo na kudai kuwa ni wa nje ya nchi, lakini
wanautumia ndani ya nchi.
"Hii inatokana na
wafanyakazi wasio waaminifu ambao wanashirikiana na wafanyabiashara hao
kukwepa kodi kwa madai kuwa mizigo hiyo ni ya nje ya nchi, huku
wakiitumia ndani ya nchi," alisema Makonda.
Makonda pia aliamuru
kufanyike uchunguzi wa tani zaidi ya 1,700 za sukari za mfanyabiashara
huyo ambazo ziliingizwa nchini kwa ajili ya kutumika viwandani.
Katika hatua nyingine
Ofisa Forodha kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) aliyejulikana kwa
jina la Ambrose Bahati, alishindwa kumtajia Makonda siku ambayo kontena
hizo zilianza kuingizwa kwenye bandari kavu hiyo licha ya mamlaka hiyo
kuwa na ofisi kwenye ICD hiyo.
"Kontena hizi ni nyingi sana hivyo ni ngumu kujua zote ziliingia lini," alisema Ofisa huyo wa TRA.
Mmoja wa maofisa wa ICD hiyo (jina linahifadhiwa) alisema,sukari hiyo iliagizwa hapo ikiwa inasafirishwa kupelekwa Uganda.