Thursday, April 28, 2016

WATAKIWA KUEPUKA ANASA KWA KUHIFADHI CHAKULA.

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO



JAMII katika Kata za Mwaluguru,Mwakata,Mwanase,Isaka na Jana,katika Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama,wameaswa kutorubunika na tamaa za mpito,kwa kuuza mazao yao,badala yake wanatakiwa kuhifadhi chakula kinachotosheleza familia zao huku wakiuuza ziada kwa ajili ya kufanyia shughuli za Kimaendeleo.

Agizo hilo lilitolewa na Afisa Tarafa wa Isagehe,Mwalimu Reuben Kadigi,kwa Madiwani,Maafisa Watendaji wa Kata,Vijiji,Viongozi wa Serikali za Vijiji,Vitongoji na vyombo vya usalama katika Kata hizo,ambapo alisema kumekuwepo tabia ya jamii kutumia pasipo uangalifu mazao yao,kwa kuuza kisha kufanya anasa.

Mwalimu Kadigi,alisema  Kata hizo  hupata zao la mpunga kwa wingi,lakini kutokana na  kutokuwa makini katika suala la uhifadhi, hususani Wanaume kuuza kwa lengo la kufanya anasa pasipo kuangalia mahitaji   katika familia zao,husababisha kuwa na mahitaji ya chakula  toka serikalini.


“Chakula cha ziada ndicho kiuzwe kwa maslahi ya familia, si kwa lengo lililozoeleka   kwa viongozi wa Kaya,pesa kufanyia anasa za ngono,ulevi uliokithiri pasipo kutambua wanazitumbukiza familia zao katika njaa siku za usoni,hivyo jitihada zifanyike kudhibiti hali hiyo,”alisema Kadigi.

Kwa upande wake Diwani wa Kata ya Isaka,Dr.Gerald Mwanzia,alisema ili jamii kuepuka njaa ni vyema ikapatiwa elimu ya kina katika uhifadhi wa chakula,kwa kutambua kiwango  kinachohitajika katika familia zao kwa idadi ya watu katika Kaya kwa mwaka mzima.  

Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwakata,Haji Omari,alisisitiza elimu kutolewa kwa wanaume wenye mfume dume ambao hujisahau kipindi hiki kwa kuuza vyakula kwa lengo la kujitumbukiza katika starehe,huku akitaka sensa ifanyike ili kubaini kila kaya imepata kiwango gani cha mazao.

Hata hivyo Afisa Mtendaji wa Kata ya Mwalugulu,Wiliam Kashindye,hakuafikiana na fikra hizo kwa madai zimechelewa kutokana na baadhi ya jamii kuuza mazao yao yakiwa shambani kwa baadhi ya wafanyabiashara kwa lengo la kujipatia fedha za kujikimu.

Nae Diwani wa Kata ya Mwakata,Ibrahimu Sixberth,alisema suala la uhifadhi chakula linahitaji usimamizi wa dhati kutoka kwa Maafisa Watendaji wa Vijiji na Kata kwa kuwajibika  kubaini kiwango cha mazao kila  Kaya kusudi itakayobainika kuuza   isije kupatiwa msaada pindi mahitaji hayo yatapotokea.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesisitiza kutumia vyema mvua za masika ili kupata mavuno mengi ya mazao na kutishia kumuajibisha Mkuu wa Mkoa pindi eneo lake litabainika kuwa na njaa ilhali kulikuwa na mvua za kutosha.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI