KAMANDA wa Polisi Mkoa wa
Mwanza,Kamishina Msaidizi Mwandamizi (SACP),Ahmed Msangi,amewaamuru askari
Polisi mkoani Mwanza,kuua mtu yeyote atakayedaiwa kuwa ni jambazi.
Msangi
ambaye amehamia mkoani humo akitokea Mbeya, ametoa kauli hiyo wakati
akizungumza na maofisa usalama na polisi wa vyeo mbalimbali baada ya
kukabidhiwa rasmi ofisi hiyo na SACP, Justus Kamugisha.
Msangi ametoa kauli hio siku chache
baada ya John Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza kusema kwamba, Kamugisha alikuwa
mzigo kwenye jiji hilo kutokana na kushindwa kukabiliana na ujambazi.
Katika kipindi cha miezi miwili ya
Machi na Aprili mwaka huu, matukio saba ya uhalifu wa kutumia silaha za moto
umeripotiwa na katika matukio hayo watu sita walipoteza maisha.
Msangi amesema kuwa, anawashangaa
polisi wanaoshindwa kutumia silaha zao kuwaua watu wanaodaiwa kuwa majambazi na
kusababisha vitendo vya uhalifu kuendelea kushamiri jijini humo.
“Tumieni na nyie bunduki zenu kuua
watu ambao ni majambazi, haiwezekana uwe na silaha halafu unaacha kuchukua
hatua za haraka za watu ambao wanasababisha mauaji na uporaji wa mara za raia,”
amesema Msangi.
Msangi alisema, Jiji la Mwanza miezi
michache iliyopita limetikiswa na matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha
yanayoambatana na mauaji ya raia, kujeruhi na uporaji wa mali zao.
Alisema kuwa, polisi wanapaswa
kufanya kazi zao kwa kujiamini na kuacha kufanya kazi kwa mazoea.
Kamanda Kamugisha akikabidhi ofisi
hiyo aliwahimiza polisi kufanya kazi kwa weledi na kwa kuzingatia maadili ya
jeshi hilo bila kumuonea mtu yeyote yule.