MAITI
ya Janeth Bambalawe(65)iliyozikwa kimamosa Usangi,Mwanga,mkoani
Kilimanjaro,imerejeshwa jijini Dar Es Salaam na kuzikwa Yombo jana katika
makaburi ya Kipunguni Mashariki.
Mwili wa Janeth ambao ulizikwa kwa taratibu
za dini ya Kiislamu mkoani Kilimanjaro,ulipowasili jijijini Dar Es Salaam jana
uliagwa na familia kwa misa ya Kikristo na baadaye kuzikwa kwa mujibu wa imani
ya dini hiyo.
Ndugu wa marehemu Janeth walibaini kutokuwapo
kwa maiti ya ndugu yao huyo baada ya kufika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili
(MNH)kwa ajili ya kuuchukua mwili,lakini waliukosa na ndipo ilipobainika maiti
yao ilichukuliwa kimakosa na familia nyingine(ya Amina Msangi)na kwenda kuzikwa
Usangi.
Uongozi wa Hospitali ya Muhimbili kwa
kushirikiana na Jeshi la Polisi,juzi walilazimika kusafiri hadi mkoani
Kilimanjaro na kuamua kuifukua maiti ya Janeth na kuirejesha Dar Es Salaam ili
ikabidhiwe kwa ndugu zake.
Wakati ikifukuliwa,maiti hiyo tayari ilikuwa
imekwisha kufukiwa na kukaa kaburini siku tatu,lakini katika hali ya kushangaza
mwili huo ulikutwa katika hali nzuri na kurejeshwa Jijini Dar Es Salaam.
Marehemu Janeth aliugua na kufikishwa
hospitalini hapo April 4,akitokea hospitali ya Amana na kulazwa wodi namba 2 Mwaisela
na marehemu Amina(76),alifikishwa hospitalini hapo April 6 akitokea hospitali ya
Temeke na kulazwa wodi namba 12 Kibasila,lakini wote walifariki dunia Aprili 8
na kuhifadhiwa katika Jokofu moja.
Akizungumzia tukio hilo msemaji wa familia hiyo,Peter
Mkude,alisema familia imeingia gharama kwa kuendesha msiba kwa siku tatu
zaidi,wakati wakisubiri maiti kurejeshwa jijini Dar Es Salaam.
Hata hivyo,alisema jana walipokea mwili wa
marehemu,majira ya saa 3 asubuhi ukiwa katika hali nzuri na baadaye kwenda
kuuzika kwa taratibu za Kikristo.
Kutokana na tukio hilo,Mkurugenzi wa Huduma
za Tiba Shirikishi wa MNH,Dk.Praxeda Ogwenyo,alisema Hospitali ya Muhimbili
italipa gharama za msiba huo pamoja na usumbufu kwa familia yake.
“Hospitali italipa gharama zilizotumiwa na
familia kwa siku tatu kuanzia Jumatatu hadi Jumatano.Tumewaomba watuletee risiti
kama zipo,kwasababu hatuwezi kuwalipa hivi hivi,lazima tukamilishe taratibu,”alisema
na kuongeza:
“Tumelazimika kuwalipa fidia kwa sababu suala
hili ni nyeti na limeiweka familia katika kipindi kigumu sana,”alisema
Dk.Ogwenyo.
Dk.Ogwenyo alisema waliwatuma wafanyakazi
watatu kwenda kuichukua maiti iliyozikwa kimakosa na kwamba wafanyakazi hao
walilipwa gharama za kujikimu ( Per diem) na gharama za mafuta za gari la
kubebea wagonjwa.
“Hao wafanyakazi walilipwa per diem
Sh.300,000 kila mmoja,mafuta ya gari Sh.240,000 na fedha za tahadhari
Sh.200,000,”alisema Dk.Ogwenyo.
Mume wa marehemu.
Akizungumzia tukio hilo,mume wa marehemu
Janeth,Theodore Chivumile (69),alisema hatalisahau tukio hilo,kwani lilimfanya
akose amani kwa muda mrefu hadi walipouona mwili wa mkewe,kisha kuuzika.
Chivumile ambaye ameishi na mkewe kwa miaka
40,alisema kitendo cha mkewe kuzikwa na kukaa kaburini siku tatu na kisha
kufukuliwa,kimezidisha machungu katika familia yake.
“ Muhimbili wanapaswa kujifunza kwa sababu
hii si mara ya kwanza tukio kama hilo kutokea.Kwakweli linaleta simanzi sana,”alisema
na kuongeza kuwa,mkewe ameacha watoto wanne na mjukuu mmoja.
CHANZO CHA HABARI GAZETI TANZANIA DAIMA.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI