![]() |
Jenister Mhagama. |
SHIRIKA
la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) shughuli zake kudorora kwa siku 15 kutokana na kutokuwa na Mkurugenzi
Mkuu,baada ya aliyekuwa akishika wadhifa huo,Dk Ramadhan Dau kuteuliwa kuwa
balozi na kuacha mara moja shughuli za kila siku za taasisi hiyo.
Rais John Magufuli alimteua Dk Dau kuwa balozi Februari 15, sambamba na makada wengine wawili wa CCM, Dk Asha Rose Migiro na Mathias Chikawe, akisema vituo vyao vya kazi vitajulikana baada ya taratibu za kidiplomasia kukamilika.
Kufuatia uteuzi huo, NSSF imekuwa ikijiendesha bila ya kiongozi mkuu,ama kupatikana anayekaimu nafasi hiyo hatua ambayo kwa taarifa za ndani ya shirika hilo linalojihusisha na hifadhi ya jamii nchini,kubainisha kudorora kwa ufanisi wa shughuli katika Shirika hilo.
Miongoni mwa mambo hayo ni ufunguzi wa Daraja la Kigamboni jijini Dar es Salaam ambalo lilitakiwa lianze rasmi kutumika Machi Mosi, ununuzi wa magari ya ofisi za mikoa, mkutano wa wanachama wa mwaka pamoja na wiki ya NSSF ambayo hujumuisha mambo mbalimbali, kama shughuli za kijamii, maonyesho ya huduma za NSSF na michezo.
Juhudi za kumpata Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Jenister Mhagama, anayehusika na mifuko ya hifadhi ya jamii hazikufanikiwa. Pia, Katibu Mkuu Kiongozi Ombeni Sefue, ambaye amekuwa akitoa taarifa za uteuzi unaofanywa na Rais, hakupatikana.
Wiki iliyopita, Balozi Sefue alisema maswali kuhusu uteuzi wa kaimu yaelekezwe kwa Mhagama, ambaye alieleza wakati huo kuwa utaratibu wa kuimpata kaimu unaendelea.
Kwa mujibu wa ripoti ya fedha ya mwaka 2011, shirika hilo lilikuwa na wanachama 501,218, kati yao wafanyakazi waliosajiliwa waliongezeka kutoka 17,666 hadi 18,779, sawa na ongezeko la asilimia 6, huku michango ikiongezeka kutoka Sh300.08 bilioni hadi Sh356.5 bilioni kwa mwaka, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18.8.
Kwa mujibu wa muundo wa uongozi wa NSSF, Mkurugenzi Mkuu ndiye kiongozi mkuu wa shirika akiwa na wakurugenzi wanane chini yake;
Wakurugenzi hao wanahusika na uendeshaji (DO); utawala na rasilimali watu (DHRA); mipango, uwekezaji na miradi (DPIP); fedha (DF); teknohama (DIT); ukaguzi wa ndani (DIA); uthibiti na usalama wa mali (DARM) na huduma za kisheria (DLS).