Kauli hiyo imesababisha tafrani kwa
muda mahakamani baada ya wasikilizaji waliokuwa wamening’inia katika madirisha
ya Mahakama ya Wilaya ya Kahama,kunakofanyika kikao hicho cha Mahakama Kuu
Kanda ya Shinyanga,kujikuta wakishangilia kwa nguvu.
Katika Mahakama hiyo ambapo kesi
hiyo ya kupinga ushindi imeanza kusikilizwa na Jaji Moses Mzuna kutoka jijini
Dar Es Salaam,imevuta hisia ya wakazi wa mji wa Kahama wanaojitokeza
kusikiliza,lakini wamekuwa wakiathiriwa na udogo wa chumba cha Mahakama,na
kusababisha waning’nie madirishani.
Mbunge huyo wa zamani wa Jimbo la
Kahama,Lembeli akiwa katika mahojiano baina yake na Mwanasheria wa
Serikali, Castuce Ndamugoba, anasema alikuwa na uhakika wa Ushindi kwa
asilimia 95 katika nafasi ya Ubunge wa Jimbo la Kahama Mjini iwapo taratibu za
Tume ya Uchaguzi zisingekiukwa na Serikali.
Lembeli anasema Serikali ilitumia nguvu
na vitisho dhidi ya wafuasi wake na wanachama wa vyama vinavyounda Umoja wa
katiba “UKAWA”ambavyo vilikuwa vinamuunga mkono katika Uchaguzi huo.
Mwanasheria wa Serikali, Ndamugoba
alimtaka Lembeli,aithibitishie mahakama juu ya kauli yake hiyo na vigezo
alivyotumia kuamini kuwa alikuwa na uhakika wa ushindi huo.
Lembeli alijibu tathimini ya vikao
vyake vya ndani baada ya Mikutano ya Kampeni ndivyo vilivyomthibitishia ushindi
hususani mikutano yake kuwa na wasikilizaji wengi.
Hata hivyo Mwanasheria wa Serikali
alihoji ni vipi alitambua wahudhuriaji katika mikutano yake ya Kampeni kama ni
wafuasi wa Chadema anaodai kumuunga mkono na hapakuwepo wafuasi wa chama
kingine na kwamba waliokuwa wakijaa katika mikutano hiyo walikuwa ni wafuasi
wake?
Lembeli alisema aliwatambua kutokana
na nembo ya chama chake walizokuwa nazo katika uhudhuriaji wa mikutano yake,kuhusu
kuwa wafuasi wake alimthibitishia kwa kumueleza atazame umati wa watu
uliojazana mahakamani kusikiliza shauri hilo,dalili inayodhihirisha anakubalika.
Mwanasheria wa Serikali alihoji kuwa
iwapo wafuasi hao waliojitokeza mahakamani hapo ni wafuasi wake?Lembeli
hakusita kutamka ni wafuasi wake na kusababisha kuibuka kwa makofi
yaliyoambatana na shangwe kutoka kwa wasikilizaji hao na kusababisha Askari
Polisi kutoka ndani ya mahakama na kuwatuliza wafuasi hao,ambao baadhi yao
walianza kutimka baada ya kubaini wametenda kosa.
Lembeli jana alikuwa akitoa maelezo
yake binafsi yaliyomfanya afungue kesi hiyo ambayo madai mengine aliyowakilisha
mahakamani hapo ni matumizi mabaya ya Serikali wakati wa Uchaguzi,ambapo
aliyekuwa Mkurugenzi wa Uchaguzi katika Jimbo la Kahama,alihamishwa akiwa
tayari na kiapo cha kusimamia Uchaguzi huo.
Madai mengine aliyowakilisha jana ni
pamoja na kuhamishwa kwa viongozi wakubwa wa wilaya wakati uchaguzi ukielekea
mwishoni,ambao waliohamishwa ni pamoja aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo,Benson
Mpesya pamoja na Mkuu wa Polisi wa wilaya aliyehamishwa kabla ya siku sita
kufanyika kwa Uchaguzi huo.
Aidha kufuatia hali hiyo,Lembeli
alisema baada ya kuhamishwa kwa viongozi hao,ambao ni wajumbe wa Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya wilaya,mambo yalianza kubadilika ikiwa ni pamoja na
kukamatwa hovyo kwa wafuasi wake wakiwemo mawakala wake walikamatwa na Polisi
siku ya kuamkia Uchaguzi.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI