SERIKALI imepiga marufuku
kwa wazazi kuozesha wanafunzi wa kike kwa nia ya kupata ng’ombe na kwamba
kuanzia sasa, Ofisa Mtendaji wa Kijiji au wa Kata ambako itagundulika kuwa
msichana ameozeshwa au kupata mimba ataswekwa ndani na kufungwa jela.
Hayo yalisemwa juzi na
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,wakati akiweka jiwe la Msingi la vyumba vitatu vya
maabara katika Shula ya Sekondari Budalabujiga wilayani Itilima,mkoani
Simiyu,kwa kutoa onyo kwa wazazi na walezi wenye kuozesha wanafunzi,
hawataachwa na mkono wa sheria.
Majaliwa alisema Serikali
haina mzaha katika suala la elimu na kwamba imedhamiria kuhakikisha kila mtoto anapata
elimu hivyo ni jukumu la maofisa hao kuhakikisha wasichana wanasoma hadi
kufikia ngazi ya chuo kikuu na zaidi.
“Nasikia hapa Itilima
wazazi wanawaozesha watoto wao ili kupata ng’ombe…jambo hili ni marufuku. Mtoto
wa kike anapoanza chekechea tunataka amalize hadi chuo kikuu. Acheni kabisa
mambo haya (ya kuozesha).” Alisema Waziri Mkuu na kuongeza:
“Kwenye eneo hili hatuna
mzaha. Watendaji wa kata na vijiji ambao eneo lao wanafunzi watapata ujauzito,
unajua na hukuchukua hatua, na wewe tunakutia ndani na tunakufunga.”
Waziri Mkuu alisema
watendaji hao wanapaswa kushirikiana na walimu wakuu na wakuu wa shule
kuhakikisha kuwa wasichana wanakuwa salama.
“Lakini wazazi na walezi
nao hatutawaacha, wanaokatisha masomo wanafunzi watachukuliwa hatua. Hatuwezi
kuona wasichana wakikatizwa masomo kwa sababu zinazoweza kuzuilika,” alisisitiza.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi
Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Itilima, John Lyimo, gharama za ujenzi wa
maabara hizo tatu za Kemia, Fizikia na Baolojia ni Sh 233,338,000 na tayari
zimetumika Sh 180,954,400 zilizotoka halmashauri, wananchi na nguvu kazi pamoja
na wadau wa elimu.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI