IMEFAHAMIKA jamii kupenda vyakula vyenye sukari nyingi huku ikikosa Elimu ya Kinywa na Meno,ndio chanzo cha watoto wengi wenye umri chini ya miaka kumi,kung’olewa meno,na asilimia 90 wenye zaidi ya miaka 30 kutokuwa na meno 32.
Hayo yalielezwa na Mratibu wa Mafunzo ya Kinywa na Meno kutoka
Shirika lisilo la Kiserikali la Bridge2Aid,Innocent Bikere,ambapo alibainisha
hali hiyo inawaathiri kwa kiwango kikubwa jamii inayoishi vijijini,kutokana pia
kutopatikana huduma ya kinywa na meno kwa wakati.
Bikere alisema jamii ya vijijini inapenda kutumia vyakula na vitu
vyenye sukari nyingi huku kwa kipindi cha zaidi ya miaka 15,ikiwa haina utamaduni
wa matumizi ya mswaki kwa ajili ya afya ya vinywa vyao,hivyo kusababisha kuwa
na matatizo ya meno yao kuuma na mengine kuoza.
.
Alisema Shirika lake lenye makao makuu yake jijini Mwanza,baada ya
kufanya utafiti na kuona Wizara ya Afya haiweki kipaumbele katika Huduma ya
kinywa na meno,liliomba ufadhili katika kampuni ya ACACIA kupitia Mgodi wa
dhahabu wa Bulyanhulu na kufanikisha kutoa meno watu 800 huku asilimia 30 ikiwa
ni watoto chini ya miaka kumi.
Kwa upande wake Dk. Helen Young, kutokana nchini Uingereza ambaye
ameongoza jopo la Madaktari 12 kutoka nchi hiyo, alisema lengo lilikuwa kutoa
Elimu ya usafi wa Vinywa kwa Matabibu katika Halmashauri ya Msalala wilayani
Kahama.
Dk. Young alisema katika mafunzo yao kwa vitendo waliwahitaji wananchi
wenye meno mabovu wafike kwenye vituo vilivyopangwa vya Lunguya na Bugarama,
kupata Elimu hiyo ya Usafi wa Vinywa na kuwapatia tiba kwa meno
yaliyotoboka,lakini walilazimika kung’oa baada ya kubaini yameoza.
Nae Meneja wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu,Graham Crew alisema
kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Kampuni ya ACACIA,imefadhili mradi huo ili
kuwasogezea huduma hiyo wananchi wanaoishi katika maeneo yaliyo jirani na
Mwekezaji huyo,ili kupatiwa huduma ya matibabu ya meno.
Katika zoezi hilo, jumla ya Matabibu 6 katika Halmashauri ya
Msalala wamepatiwa mafunzo ya huduma ya Kinywa na wakati wa mafunzo hayo, idadi
kubwa ya wananchi waliofika kupewa Elimu hiyo walibainika meno yao yameoza kutokana
na utunzaji hafifu wa kinywa.