![]() |
KATIBU Mkuu Kiongozi,Balozi Ombeni Sefue. |
IKULU ya Rais Dk.John Magufuli imeingia katika mgogoro na wasanii
wa sanaa za uchoraji baada ya kudaiwa kushindwa kulipa deni lao la Sh.Milioni
53.6.
Wasanii hao 19 wanadai
deni hilo lililtokana na kazi waliyoifanya ya kuchora picha mbalimbali ambazo
zinapamba Ikulu,walizopeleka Agosti mwaka jana
wakati Rais Mstaafu Jakaya Kikwete akiwa madarakani.
Wasanii hao na kiasi
kianchodaiwa na kila mmoja kwenye mabano ni Cuthbert Semgoja{Sh.Milioni
6.8},Florian Kaija{Sh.Milioni 3},Evarist Chikawe{Sh.Milioni 2.8},Haji
Chilonga{Sh.Milioni 6.6}Robino Ntila{Sh.Milioni 3.6}na Vita
Malulu{Sh.Milioni8.9}.
Wengine ni Masoud
Kibwana{Sh.Milioni 3.5},Said
Ray{Sh.Milioni 1},David Kyando{Sh.Milioni 2},Paulo Ndunguru{Sh.Milioni
1.5},Thobias Minzi{Sh.Milioni 4.1},Lutengano Mwakisopile{Sh.Milioni
1.2}Yussuf Khamis Yussuf{Sh.Milioni
1.6}na Ali Ali Kigata{Sh.650,000/-}.
Pia wamo Hamza Mohamed
Ausi{Sh.800,000/=},Suleiman Rashid{Sh.Milioni 1.8},Ismail Mbarak
Mselem{Sh.800,000/-} na Claud Chatanda{Sh.Milioni 2.2},ambao wote kwa ujumla
wanadai Sh.Milioni 53.6.
Katika harakati za kudai
haki yao,wasanii hao wamesema wamekuwa wakifanya juhudi za kukutana na viongozi
mbalimbali wa Ikulu tangu wakati wa Rais Kikwete hadi sasa chini ya Rais
Magufuli bila mafanikio.
Akizungumza na Tanzania
Daima jana jijini Dar Es Salaam,Mwenyekiti wa Wasanii hao,Lutengano
Mwakisopile,tangu walipowasilisha kazi zao ni zaid ya miezi tisa sasa,lakini
hawajalipwa fedha zao.
Alisema waliahidiwa
kulipwa fedha hizo kabla ya Uchaguzi Mkuu mwaka jana,lakini wamekatishwa tama na
majibu yasiyoridhisha kutoka kwa wahusika Ikulu.
“Ahadi tuliyopewa ni
kwamba tungelipwa kabla ya Uchaguzi mkuu mwaka jana na kumekuwa na mlolongo wa
ahadi unaojirudia rudia kwamba malipo yenu yanaandaliwa.Kwa vile mawasilano
yetu na Ikulu kuhusu deni letu yamezidi kufifia,tumeona njia bora ni kukutana
na vyombo vya habari ili watusaidie kupaza sauti zetu,”alisema Mwakisopile na
kuongeza:
“Imefikia hatua simu zetu
hazipokelewi na hata ukituma ujumbe mfupi wa maneno hupati majibu.Hatukukata tamaa,tukaamua
kwa pamoja tujaribu kupiga simu kwenye Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi,Balozi
Ombeni Sefue,lakini maelezo tuliyopewa yanakatisha tama,mwisho wake hakukuwa na
majibu yanayoridhisha hadi leo hii.”
Mmoja wa wasanii hao ambae
aliwahi kuwa Mjumbe wa Baraza la Sanaa la Taifa(Basata),ambaye aliomba hifadhi
ya jina lake,alisema kama Ikulu isipotekeleza malipo yao wataiburuz mahakamani.
Idara ya Maelezo lawamani
Mwenyekiti huyo wa
wasanii,alieleza jana walifika katika Ukumbi wa Idara ya Habari(Maelezo)kwa
lengo la kutaka kuzungumza na wanahabari,lakini uongozi wa Idara hiyo uligoma
kuwapa nafasi.
Alisema walipofika majira
ya saa nne kutaka kulipia gharama za ukumbi,walikutana na mmoja wa watendaji wa
idara hiyo ya serikali ambaye alikataa kuwapa nafasi baada ya kujua azima ya
mkutano wao.
“Kwa kuwa tunafahamiana na
baadhi ya waandishi ambao huwa tunafanya nao kazi tukiwa na maonyesho
walitushangaa kutuona nje ya Ukumbi wa Maelezo,ndipo wakatuita tukaanza kueleza
kilio chetu,”alisema Chikawe na kuongeza:
Lengo letu ni kupata haki
yetu ya malipo ya kazi tuliyofanyia Agosti mwaka jana,kila mmoja wetu ana idadi
yake ya picha,makubaliano yetu yalikuwa tulipwe fedha kabla ya Uchaguzi Mkuu
uliofanyika Oktoba 25,mwaka jana lakini hadi sasa hatujalipwa haki zetu,”alisema.
Ufafanuzi
wa Ikulu.
Kaimu Mkurugenzi wa
Mawasiliano – Ikulu,Gerson Msigwa,alikiri kuwapo kwa madai hayo nakuongeza kuwa
wasanii hao wapo katika mazungumzo na watu wa manunuzi ili kupitia gharama
wanazodai kwa lengo la kujua kiasi halisi wanachodai.
“Ni kweli hayo madai yapo
na waliyaleta Novemba mwaka jana,lakini kiwango ambacho walikidai ni kikubwa
hakilingani na uhalisia wa deni,”alisema Msigwa.
Alisema Ikulu imeshangazwa
na hatua ya wasanii hao kuamua kwenda kwenye vyombo vya habari,huku ikijua fika
kwamba suala lao linashughulikiwa.
“Kitendo walichokifanya cha
kuwa katika mazungumzo halafu wanatoka kwenda kuzungumza na vyombo vya habari
ni cha kusikitisha sana,kwani hata walipomaliza kuzungumza na waandishi
leo(jana){Februari 24,2016},walikuja tena hapa Ikulu sasa hatujui wana maana
gani.”
Kuhusu deni lao alisema
mara baada ya watu wa manunuzi wa Ikulu na wasanii hao kumaliza
majadiliano,fedha zao zitalipwa mara moja,kwani Ikulu haiko tayari kumdhulumu
mtu.
Chanzo cha Habari ni gazeti la Tanzania Daima.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI