HATIMAYE
kilio cha Watanzania kilichojitokeza baada ya Serikali kusitisha matangazo ya
moja kwa moja kutoka Bunge
la Tanzania kupitia Shirika la Utangazaji nchini (TBC),kwa madai ya ukosefu wa fedha,kimepata ufumbuzi.
Suluhisho hilo kwa Watanzania limetoloewa na Mfuko
wa Vyombo vya Habari nchini (TMF),lililodai kuwa tayari kurejesha haki hiyo ya
msingi kwa Wananchi kwakuwa tayari kutoa
fedha zinazohitajika na TBC.
Akiongea hivi karibuni na Wahariri wa Vyombo vya
Habari,Jijini Dar Es Salaam,Mkurugenzi Mtendaji wa TMF,Ernest Sungura,alidai
pindi Serikali itaafiki pendekezo lao,wananchi wataendelea kunufaika na vikao
vya moja kwa moja vya bunge,na si utaratibu ilioanza wa kunakili baadhi ya
sehemu na kisha kuoneshwa usiku.
Mkurugenzi Mtendaji huyo wa TMF,aliwaeleza wahariri
wa habari na serikali kupitia mwakilishi wake Assah Mwambene ambaye ni
Mkurugenzi wa Habari Maelezo kwamba, taasisi hiyo imejipanga kutoa gharama
inayohitajika ili kuhakikisha Watanzania wanaendelea kupata matangazo ya moja
kwa moja kutoka bungeni kupitia TBC.
Sungura alisema taasisi hiyo imaemaua maamuzi hayo
kutokana na kwamba miongoni mwa malengo ya mfuko huo ni pamoja na kuleta
mabadiliko katika tasnia ya habari,nchini kwa kuhakikisha wananchi wanapata taarifa kwa
wakati.
Januari mwaka huu, Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo,Nape Nnauye, alitoa ufafanuzi bungeni kuhusu hatua ya serikali
kusitisha matangazo ya moja kwa moja ya bunge kupitia TBC,huku akianisha sababu
alizozieleza ni pamoja na kuwepo kwa gharama kubwa katika kurusha matangazo
hayo.
Nnauye alisema gharama ya Sh. 4.2 bilioni
zinazotumika katika uendeshaji wa matangazo hayo ya moja kwa moja kwa mwaka,huku
kuwepo kwake kukidumaza ufanisi wa shughuli maofisini kutokana na watumishi wa serikali kushabikia bunge badala
ya kuendelea na kazi ofisini.
Hatua ya serikali kusitisha matangazo hayo iliibua
mjadala mkubwa bungeni huku Zitto Kabwe, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo)
akilitaka bunge kusitisha shughuli zake ili kujadili taarifa hiyo ya serikali.
Nje ya bunge mjadala huo uliendelea bila kupatikana
kwa ufumbuzi ambapo TMF imedhamiria kugharamia matangazo hayo ili kuruhusu
wananchi kuendelea kupata matangazo hayo kupitia TBC.
Katika mkutano huo, Mwambene amesema kwamba,
serikali itafikiria namna ya kupeleka maombi TMF ya uwezeshwaji katika
maandalizi ya miswada miwili ya sheria za habari ili kupitisha sheria zenye
matakwa ya wadau.
Kuhusu hilo, Sungura amesema taasisi yake iko tayari
kuisaidia serikali kwenye mchakato huo na hata kuitisha kongamano kubwa la
wadau.