MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Kahama Anderson Msumba,awatimua
wazazi katika madawati huku akipiga marufuku katika kipindi cha masomo jamii kuyatumia
kwenye mikutano na vikao mbalimbali,kwakuwa kitendo hicho ni kinyume na haki
anazostahili kupatiwa mwanafunzi.
Kauli hiyo aliitoa katika Kata ya
Iyenze,wakati akipokea madawati 60 kutoka Ushirika wa Wachimbaji wadogo wa
Isalenge Iyenze Gold Mine wa wilayani Kahama,ambapo alisema ni kinyume cha haki
za binadamu kutumia madawati yanayohitajika kutumiwa na wanafunzi kipindi cha
masomo.
Msumba alisema tabia hiyo
imezoeleka kwa jamii kukatisha masomo ya wanafunzi kwa ajili ya kutumia
madawati kwa kushughuli zao za kijamii na kutoa agizo kwa Maofisa Watendaji wa
Kata kusimamia agizo lake la kuzuia madawati kutumika na wazazi ambao wamekuwa
wakaidi kuwatengenezea mazingira bora ya kusoma vijana wao.
“Inashangaza wazazi hapa
wamekusanyika kuja kushuhudia wahisani wakikabidhi dawati huku wakikalia dawati
zilizopo 30 na kusababisha vijana wetu kuendelea na masomo wakiwa wameketi
chini kuanzia leo marufuku na ninakuombeni myapeleke madarasani nasi tutasimama
kuendelea na jukumu lililo mbele yetu,”alisema Msumba.
Aidha Mkurugenzi huyo alitumia fursa hiyo kumuagiza Afisa Elimu wa
Halmashauri ya Mji kuhakikisha shule zote hakuna kutoa madawati nje kwa ajili ya
mkutano wowote,huku jamii ikishindwa
kuchangia madawati ili kuwezesha vijana kusoma katika mazingira mazuri yatakayowawezesha kufanya vyema katika mitihani yao.
Katika makabidhiano hayo Mkurugenzi wa
ushirika wa Isalenge Iyenze Gold Mine,James Belela,
alisema waliamua kujikita kutoa msaada wa madawati, kutokana na hali mbaya
katika shule za Kata hiyo,ambapo waliamua
kutoa dawati 40 katika shule ya Msingi Iyenze na 20 katika Shule ya Msingi Isalenge.
Awali katika hafla hiyo, Mwalimu Mkuu wa
shule hiyo David Joseph, alisema shule
hiyo inajumla ya wanafunzi 589 huku ikiwa na dawati 90 hali inayosababisha wanafunzi zaidi
ya mia mia tatu kutoka darasa la kwanza hadi la saba kukaa chini,hali
iliyosababisha Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Ushirika huo,Pius Gulamse
kuahidi kutoa dawati zingine 30.
Mkurugenzi Mtendaji wa
Ushirika huo,Belela alisema ushirika wake uliguswa na uhaba huo wa madawati
katika Kata hiyo ambayo ina rasilimali za madini ya dhahabu,japo kuona tatizo
hilo ni la wazazi hivyo kuamua kutoa dawati hizo 60, zilizogharimu milioni 9,200,000/= .
Pamoja na msaada huo wa
dawati pia Ushirika huo uliamua kutoa mifuko 100 ya Saruji,huku Mkurugenzi Mtendaji wa
Halmashauri ya Mji,Msumba kuamua kutoa Shilingi Milioni 12 baada ya kushuhudia wanafunzi wamekaa chini ya vumbi lililochafua nguo kutokana na kuharibika kwa sakafu,na
kiasi kingine kuagiza kutumika kukamilisha ujenzi wa vyoo, uliokwama uliokuwa
ukifanyika kwa nguvu za wananchi.