Wednesday, February 10, 2016

WALIMU WASTAAFU WAASWA KUTOKIMBILIA KUFANYA BIASHARA KUBWA.

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO

                                           
NAIBU Katibu CWT;Ezekiah Oluoch.
WALIMU wanaostaafu wameonywa kutokimbilia kufanya biashara za kifahari sambamba na kununua magari kwa pesa zao za mafao yao,badala yake ni vyema wakanunua ng’ombe wa maziwa na kujikita katika biashara  ya kuuza maziwa,ambayo itasaidia kuwafanya waendelee kuishi maisha mazuri.
 
Onyo hilo lilitolewa katika hafla ya kuwaaga walimu nane waliostaafu katika wilaya ya Kahama,na Mwenyekiti wa Chama cha Walimu {CWT}katika Halmashauri ya Ushetu,Juma Nyakanyange,ambapo alisema wastaafu wasipotumia mafao yao vizuri kwa kufanya biashara wanazomudu watakakuwa na maisha magumu.
 
Nyakanyange aliwakumbusha kuwa muda wao mwingi wa maisha wameutumia katika utumishi wa umma,hivyo kujikita katika biashara kubwa za kumiliki maduka,hoteli ama za magari hawataweza kutokana na ushindani mkubwa wa kibiashara uliopo unaostahili kuendana na umri,na kujitumbukiza katika biashara hizo ni kujitakia umaskini.
 
“Muda mwingi mmeutumia katika utumishi,ni vyema sasa mkafanya biashara   inayolingana na umri wenu ambayo haitawasababishia maradhi ya BP,na inayostahili ni ng’ombe wa maziwa,na ambao bado tuko katika utumishi tuanze kujiandaa na maisha ya ustaafu,”alisema Nyakanyange.
 
Akiongea kwa niaba ya Katibu Mkuu CWT Taifa,Mwenyekiti wa chama hicho Mkoani Shinyanga, George Nyangusu,alisema walimu wengi  wamekuwa wakiishi maisha magumu,mara baada ya kustaafu kutokana na kutokuwa na mpango mzuri wa matumizi ya fedha za mafao ambazo hulipwa  walimu hao wanapostaafu.
 
“Ni aibu baada ya kustaafu kuwa na maisha mabaya  ya ufukara wakati umefanya kazi kubwa ya kulitumikia taifa hili ukiwa mwalimu,hivyo ni vyema walimu kuanzia sasa walimu wanaostaafu walimalize tatizo hilo kwa kuwa makini na fedha hizo na wanapaswa kuwa na mpango mzuri wa matumizi yake,”alisema Nyangusu.
 
Halfa hiyo ya kuwapongeza walimu hiyo ilikwenda sambamba na kuwazawadia walimu hao wanane kila mmoja mabati ishirini yote yakiwa na thamani ya shilingi milioni tatu na laki nne,huku wastaafu hao wakiomba uwepo utaratibu wa kuwaalika na wenzi wao katika hafla hizo kutokana na kuwa na mchango mkubwa katika maisha yao ya utumishi.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI