DIWANI Kata ya Isaka. |
BARAZA
la Madiwani wa Halmashauri ya Msalala,wilayani Kahama,limeridhia kuanzishwa kwa
Mamlaka ya Mji Mdogo wa Isaka,ili kusogeza huduma kwa wananchi na kusaidia kuboresha
mapato yatakayosaidia kupatikana maendeleo stahiki na kwa wakati sambamba na
kukuza uchumi wa Taifa.
Akiwasilisha
mapendekezo hayo katika Kikao cha Kawaida cha Baraza hilo,Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Msalala,Patrick
Kalangwa,alisema walipokea mapendekezo ya
kuanzishwa Mamlaka ya Mji Mdogo wa Isaka kutoka Kata ya Isaka kwa barua iliyowasilishwa
ofisini mwake Januari 4,mwaka huu.
Kalangwa
alisema kimsingi mapendekezo hayo baada ya kupitiwa na wataalamu yalionekana
yana tija kwa maslahi ya Taifa na wananchi wa maeneo hayo,hasa kwakuwa itasaidia
kuboresha ukusanyaji wa mapato utakaosaidia upatikanaji maendeleo kwa wakati
katika eneo hilo na kukuza uchumi wa wananchi na Taifa.
Kwa
upande wake Diwani wa Kata ya Isaka,Dr.Gereld Mwanzia,alisema kutokana na
ukubwa wa mji,rasiliamali na miundo mbinu iliyopo huku tangu mwaka 1994 ukitangazwa na
gazeti la serikali kuwa eneo la mipango miji,ni vyema ukawa Mamlaka wa Mji
Mdogo.
Dr.Mwanzia
alisema Kata hiyo ina wakazi 15,928 wakiwemo wafanyabiashara
wanaomiliki maduka ya jumla sita,rejareja 152 ,nyumba za kulala wageni 124,pia kuna ofisi za
serikali nane,za Uhamiaji,Polisi,TRA,TTCL,TRL,Bandari ya Nchi kavu na Mahakama
sambamba na uwepo wa makampuni makubwa 34 yanayojihusisha na usafirishaji na
ujenzi.
Madiwani
hao kwa kauli moja waliridhia uanzishwaji wa Mamlaka hiyo na kuanisha Kata za
Isaka,Mwanase,Mwakata,Mwaluguru na Janna kuunda Mamlaka hiyo huku wakipendekeza
Kata ya Isaka ndiyo kuwa makao makuu yake kutokana na miundo mbinu yake ikiwemo
kuwepo kwa ofisi za serikali na makampuni.
Halmashauri ya Msalala ni kati ya
Halmashauri tatu zinazounda wilaya ya Kahama,ambayo ni kubwa kwa eneo hivyo kusababisha baadhi ya
wananchi wa Kata za pemebezoni kuchelewa kupata huduma mbalimbali za kijamii.