IMEBAINIKA kwamba
chanzo cha baadhi ya Mawikili katika Mahakama mbalimbali Nchini kukimbia kesi za
Wateja wao ambazo walianza kuzisimamia
kunatokana na ucheleweshwaji wa
Mashauri
hayo kutotolewa hukumu kwa wakati,na kuwasababishia gharama kuwa kubwa tofauti
na malipo waliyolipwa.
Akiongea kwa niaba
ya Mawakali katika Kilele cha siku ya Sheria nchini Wilayani Kahama,Wakili
Msomi Kelvin Murusuri,alisema kutokana na kesi wanazowatetea Wateja wao mwenendo
wake katika Mahakama kutumia muda
mrefu kumesababisha kipato chao kushuka kwa kuhofia
kuwa na mrundikano wa kazi.
Wakili huyo
alisema kuwa kitendo cha mashauri mengi Mahakamani kuchelewa kusikilizwa kwa
wakati kunachangia kwa kiasi kikubwa katika kupunguza Morali wao wa
kufanya kazi hali ambayo inawakatisha tamaa Wateja wao wanaokwenda kutafuta
huduma kwao,huku nao kulazimika kuzikimbia baada ya gharama ya kesi
waliyokubaliana na mteja kufikia ukomo huku mwenendo wa kesi ukiwa bado mrefu.
Aidha alisema kuwa
kama kesi moja itasikilizwa kwa muda mrefu wanapata hasara kubwa kwani kazi yao
hiyo ya kutoa huduma inahitajika kwa wananchi wengi na kuongeza kuwa kwa wao
kushinda mahakamani kila siku wanapoteza wateja wengi wanaohitaji huduma
yao.
Awali akisoma
taarifa ya Mahakama hiyo mbele ya Mkuu wa Wilaya ya Kahama Vita Kawawa
aliyekuwa Mgeni rasmi katika sherehe hizo, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mfawidhi wa
Mahakama ya Wilaya ya Kahama,Evodia Kyaruzi,alisema kuwa mahakama yake kwa
mwaka jana imejitihadi katika kuhakikisha kuwa mashauri waliokuwa nayo
yanasikilizwa kwa wakati.
Kyaruzi alisema
kuwa kwa mwaka 2015 jumla ya mashauri 1105 yalisikilizwa na kupatiwa hukumu
kati ya 1218 yaliokuwepo ,huku 113 yakibaki kitendo ambacho aliwapongeza
Mahakimu pamoja watumishi wa Mahakama hiyo kwa kujitahidi katika kutoa huduma
kwa Wananchi katika maeneo mbalimbali ya Wilaya.
Hakimu huyo
aliwataka watumishi wa Mahakama kuwa wazi kwa Wananchi kuhusu kazi wanazozifanya
ili jamii iwe na imani katika uendeshwaji wa kesi zao mahakamani hapo hali
ambayo itakuwa ni changamoto kubwa kwa wananchi kuelewa sheria tofauti na
ilivyo kwa sasa.
Kwa upande wake,Mkuu
wa Wilaya ya Kahama,Vita Kawawa, alisema kuwa katika Wilaya ya Kahama kuna
tatizo kubwa kwa baadhi wa Wananchi kutozijua sheria kwa kiwango kikubwa hali
ambayo inafanya watu wengi kufika ofisini mwake kutoa malalamiko huku matatizo
yao makubwa yao yakiwa ni yale ya kisheria.