Friday, February 12, 2016

MGANGA MBARONI KWA KUMUUZIA MFANYABIASHARA MADAWA YA SERIKALI

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO

 Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Hamis Kigwangala

 JESHI la Polisi wilaya ya Kahama Mkoani Shinyanga,linamshikilia kwa uchunguzi mtumishi mmoja katika
Hospitali ya Halmashauri ya Mji Kahama,kwa madai ya kukutwa akiuza kinyume cha taratibu  dawa na vifaa tiba vya Serikali vyenye thamani ya Shilingi 106,000/-kwa mfanyabiashara wa duka la madawa.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga,Mika Nyange,alimtaja Mtumishi huyo kuwa ni Egbart Kahugya,ambapo alikamatwa akiwa katika mgahawa mmoja mjini Kahama akiwa katika harakati za kuuza kwa mfanyabiashara mmoja wa maduka ya dawa.
Kamanda Nyange alisema mtuhumiwa huyo baada ya kuwekwa chini ya ulinzi ulifanyika upekuzi katika gari yake iliyokuwa kanda ya Mgahawa huo na kukutwa na mzigo huo wa madawa,na kwamba Polisi Mjini Kahama,bado inafanya uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo kwa kuwahoji watuhumiwa wote wawili,kabla ya kuwafikisha Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria.
Kwa upande wake Mganga Mkuu katika Hospitali ya Halmahauri ya Mji wa Kahama,Bruno Minja,alishtushwa na kittendo hicho cha Tabibu Kahugya kufanya vitendo vya kibadhirifu ambapo alidai uongozi wa hospitali utachukua hatua stahiki za kimaadili juu ya mtumishi huyo.
Dk.Minja alisema tayari wamechukua hatua za kisheria kwa kufungua kesi kwa tabibu Kahugya,kwa kosa la kupatikana na dawa za serikali kinyume cha sheria kwa kufungua jalada lenye namba KAH/IR/683/2016,baada ya kujiridhisha na kuwaonya vikali watumishi wake wasiowaaminifu,kuondokana na tabia   ya wizi wa madawa na badala yake wafanye kazi kwa uadilifu.  
Mganga Mkuu huyo alisema baada ya kukamatwa kwa tabibu huyo,kwa kushirikiana na Polisi walifika Hospitalini hapo na mzigo huo na kubaini madawa hayo na vifaa tiba yapo katika makundi matatu ambapo kundi la kwanza ni dawa za serikali, la pili  ni dawa halali, na la tatu ni dawa ambazo hazijasajiliwa ambazo usajili wake ulifutwa na mamlaka ya chakula na dawa “TFDA”.
Dr.Minja alifafanua kuwa katika mzigo wa dawa za Serikali alizokamatwa nazo tabibu huyo ni aina ya Benzyl Penicillin zenye thamani ya TSh 22200/- na Hemocue HB Covettes zenye tahamani ya TShs 83800/-huku mzigo ungine ukiwa ni ule wa madawa ambayo hupatiwa kwa msaada.Na ule ambao ulifutwa na TFDA thamani yake ukiwa haijulikani.
Aidha alisema tukio hilo limedhihirisha kuwa kuna baadhi ya watumishi katika hospitali hiyo si waadirifu na hufanya kazi kwa mazoea,na kujinufaisha binafsi na kusahau maslahi ya Taifa, hali ambayo amedai haikubaliki na kama wataendelea kufanya hivyo wataishia pabaya kutokana na serikali ya sasa kutumia nguvu kubwa kuthibiti wizi wa dawa.
 Kufuatia hali hiyo Minja amesema katika serikali ya awamu ya tano lazima watumishi wabadilike kama zamani walikuwa wakiiba sasa basi waache kwa kuwa hivi sasa mikakati iliyopo ni kukomesha wizi wa dawa na vifaa tiba hospitalini,na atahakikisha katika hospitali anayoiongoza vitendo hivyo vinakoma na hatosita kuwachukulia hatua kali watumishi watakaobainika wamefanya ubadhirifu.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI