Saturday, February 20, 2016

DIWANI AKERWA NA WALIMU KUCHELEWA SHULENI.

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO

                 
MHESHIMIWA Gerlad Mwanzia.
MWENYEKITI wa kamati ya  Elimu, Afya na Maji, Halmashauri ya Msalala wilayani Kahama,mkoani Shinyanga,Gerlad Mwanzia   amefanya ziara ya kushtukia katika baadhi ya shule zilizopo katika kata ya Isaka kujionea maendeleo na changamoto zilizopo katika shule hizo.

Mwanzia ambaye pia ni diwani wa Kata ya Isaka alifanya ziara hiyo jana,katika Shule  za Msingi Bandari na Isaka pamoja na
Shule ya Sekondari Isaka.Ambapo awali alifika katika Ofisi za Kata majira ya saa 1:34 na kulazimika na kuondoka na Kitabu cha Mahudhurio ya Watumishi.

MH:Mwanzia akiondoka na kitabu cha mahudhurio
Diwani huyo aliamua kuondoka na Kitabu hicho kutokana na kuchelewa kwa watumishi katika ofisi hiyo,ambapo alikuwepo Mgambo tu ambaye ndiye alifungua ofisi  hiyo,kitendo kilichomchukiza kwakuwa alidai ni kero na kinachelewesha kutoa huduma kwa wananchi kwa wakati.

“Wananchi wanahitaji kuhudumiwa matatizo yao kwa wakati,wao wanachelewa ina kera ni vyema waache kufanya kazi kwa mazoea,awamu hii tunahitaji uwajibikaji uliotukuka ili tupate maendeleo stahiki,kitendo hiki nitakifikisha kwa mwaajiri wao ambaye ni Mkurugenzi,”Alisema Mwanzia.

Akiwa katika Shule ya Msingi Bandari alishuhudia  idadi kubwa ya  walimu  wakichelewa kufika shuleni katika muda wa kazi na kulazimu  kumwagiza mwalimu Mkuu wa Shule hiyo Pili  Hamisi  ampatie taarifa ya maelezo ya walimu kwanini wamechelewa  ifikapo Jumatatu.

WANAFUNZI wakiendelea na masomo.
Hata hivyo  Mwanzia alijionea changamoto mbalimbali katika shule hiyo,ikiwemo upungufu wa madawati,hali ambayo inalazimu wanafunzi kukaa chini pamoja na uhaba wa matundu ya vyoo  hali ambayo inatishia usalama wa afya za wanafunzi.

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo,Pili Hamisi alisema  ipo mikakati ambayo wameanza kuifanya ili kunusuru hali hiyo,hususani katika suala la mapungufu la madawati kwa kutumia fedha zilizochangwa na jamii kwa ajili ya maendeleo ya shule .

AKIANGALIA Dawati zinazotakiwa kufanyiwa ukarabati
Kwa upande wake  Mwanzia alisema ni vyema  changamoto zinazoweza kutekelezeka kwa wakati pasipo kusubiri msaada kutoka serikalini ukafanyika ili kuinusuru Shule hiyo,na kusisitiza suala la uzalendo kwa walimu katika kusimamia changamoto hizo.

Aidha katika shule ya sekondari Isaka, matokeo  mabaya  ambayo shule hiyo imeyapata ya kidato cha nne  yameonesha kumshitua  diwani huyo, kutokana na kwamba shule hiyo imefaulisha wanafunzi  19 pekee kujiunga na   kidato tano huku wanafunzi 62 wamepata  wasitani wa daraja la sifuri.

“Matokeo haya si mazuri,ni vyema mkaketi mkatafuta chanzo cha tatizo,hamstahili kulaumiana.Mkipata kiini chake ndipo mtapopata ufumbuzi wa kutatua na kuondokana na shule kufanya vibaya,”alisema Mwanzia.

AKIMSIKILIZA Mkuu wa Shule ya Sekondari
Mkuu wa shule hiyo,Daniel Kabola alieleza changamoto zilizosababisha hali hiyo,kuwa ni kutokana na utoro mkubwa uliokithiri wa wanafunzi huku jamii ikiwa na ushirikiano mdogo katika kukabiliana na hali hiyo.

Kabola alisema kuna wanafunzi wanatumikishwa na walezi wao kufanya biashara hadi nyakati za usiku hali inayoathiri uwezo wa kufanya vyema katika masomo kwa vijana hao,huku baadhi ya watoto wa kike wakijitumbukiza katika masuala ya mapenzi kwa ushawishi wa madereva wa magari makubwa ya mizigo yapelekayo bidhaa nchi jirani za Rwanda,Burundi na Kongo.

Nae Mwalimu wa Taaluma katika Sekondari hiyo,Violet Cyprian alisema wanafunzi hawapati fursa ya kurejea waliyofundishwa shuleni wakiwa nyumbani kutokana na kutumikishwa shughuli mbalimbali,jambo linalosababisha vijana kushindwa kufanya vizuri katika masomo yao.

Hata hivyo walimu hao walisema baada ya Matokeo hayo kuwa mabaya wamejipanga kufanya vyema ili kunusuru hali hiyo kwa kuhakikisha wanafundisha kwa bidii zaidi na kuongeza muda wa ziada kwa kuwaweka wanafunzi katika makundi ya mijadala na kuwapatia mazoezi zaidi ya masomo mbalimbali.

Chanzo chetu ni Boniphace Mabisilo

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI