WAANDISHI wa Habari
wameaswa kufuata taratibu zinazohusika kufika katika maeneo ya wawekezaji
hususani migodi ya dhahabu,kujionea utendaji kazi na si
kukurupuka kuandika na
kutangaza taarifa potofu juu ya Mwekezaji.
Kauli hiyo ilitolewa na
Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu,unaomilikiwa na Kampuni ya
ACACIA;Graham Crew,wakati akiongea na Waandishi wa Habari tisa kutoka mikoa ya
Mwanza na Shinyanga,waliofanya ziara kujionea utendaji kazi wa Mgodi.
Crew alisema,Waandishi wa
Habari ni washirika muhimu katika kumuunganisha Mwekezaji na jamii na kusaidia
kusukuma maendeleo ya Taifa pindi kalamu wanazotumia zikitumika kwa weledi na
kuzingatia miiko na maadili ya Habari.
Alisikitika kuona baadhi
ya waandishi kutofahamu mazingira ya uwajibikaji wa Mgodi,lakini wamekuwa
mstari wa mbele kutoa taarifa katika vyombo vya habari potofu ambazo zimekuwa
zikichochea kutokuwepo mahusiano mema na jamii inayomzunguka Mwekezaji huyo.
“Msikurupuke pindi
mnapoletewa tuhuma dhidi yetu,fanyeni uchunguzi na uandishi huo utakujengeni na
kuaminika katika jamii”,Alisema Crew.
Kwa upande wake Meneja
Ufanisi wa Mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu,Elias Kasitila,aliwasihi waandishi wa
habari kusimamia ukweli na usahihi,ili kuijengea heshima taaluma huku
akisisitiza taaluma ya habari itumike kutangaza shughuli za kijamii zilizofanywa
na Mwekezaji huyo.