Wednesday, December 16, 2015

DC KAHAMA, "HAKUNA MTIHANI ULIOVUJA"

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO

MKUU wa wilaya ya Kahama,Vita Kawawa.


SERIKALI wilayani Kahama,imekana kutokea kwa uvujaji wa mitihani ya Taifa ya kidato cha nne katika shule mojawapo Halmashauri ya Mji wa Kahama,kwa kudai ni uvumi ambao haukuwa
na lengo zuri kwa maslahi ya kielimu wilayani Kahama.

Akiongea na waandishi wa Habari,Mkuu wa Wilaya ya Kahama,Vita Kawawa, alisema baada ya kuulizwa na waandishi,alivituma vyombo vyake vya ulinzi na usalama vya wilaya,vilivyobaini katika Halmashauri tatu zilizomo wilayani mwake hakuna tukio lolote la wizi wa mitihani ya Taifa ya Kidato cha nne .

Kauli hiyo ilikuja baada ya kuwepo kwa utata kwenye tukio hilo,ambalo kwa mujibu wa baadhi ya vyombo vya habari na mitandao ya kijamii vilimnukuu   Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga,akidai polisi wilayani Kahama inawashikilia kwa uchunguzi walimu wawili kati ya 12 wa shule ya sekondari ya Anderlek Ridgers wanaodaiwa kukutwa na majibu ya mtihani wa somo la historia.


Kawawa alisema baada ya kupata taarifa hizo dhidi ya walimu wa shule  hiyo  aliviagiza vyombo vyake vya Ulinzi na Usalama,ambavyo vilianza kufuatilia kwa kina tuhuma hiyo na kubaini kuwa ni uvumi wala hapakuwa na walimu  waliosimamia mitihani hiyo ya Taifa waliokamtwa na majibu ya mitihani hiyo.

Alisema mbali ya wasimamizi hao kutokutwa na majibu,ama kubainika kuwaelekeza majibu wanafunzi pia hapakuonesha dalili ya wanafunzi wahitimu kuingia katika vyumba vya mitihani wakiwa tayari  na majibu ya somo lolote katika wilaya  ya Kahama.

“ Mimi kama Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya ya Kahama, vyombo vyangu vya ulinzi na usalama niliviagiza kufuatilia kwa kina taarifa hizo na kubaini madai hayo ni uvumi,na kwakuwa yalikuwa na lengo la kuchafua taswira ya elimu nimeviagiza kumtambua “source”wa uvumi ili sheria ichukue mkondo dhidi yake,”alisema Kawawa.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga,Justus Kamugisha,alisema suala hilo hawezi kuliongelea kwa kuwa anataraji kupata taarifa za uchunguzi kutoka kwa vijana wake ndani ya wiki hii ndipo atapoweza kulizungumzia,kama taarifa za awali zilikuwa sahihi ama ulikuwa uvumi.

Kwa upande wake,Ofisa elimu ya Sekondari katika Halmashauri ya Mji wa Kahama,Anastazia Manumbu,ambapo ndipo ilipo sekondari ambayo walimu wake walidaiwa kurushiwa majibu hayo kutoka mkoani Kagera,alisema katika mitihani ya  taifa ya kidato cha pili  na cha nne iliyomalizika Novemba 27 mwaka huu, hakukuwa na tukio lolote la walimu ama wanafunzi kukamatwa na majibu ya mitihani hiyo.

Manumbu alisema kamati yake ya mitihani ya taifa ya kidato cha pili na cha nne  ilijiridhisha wasimamizi wa mitihani walitekeleza majukumu yao kwa umakini wa hali ya juu kwa  kufuata sheria na kanuni zote za baraza la taifa  la mitihani na kumaliza kwa amani na hakuna msimamizi aliyehojiwa ama kushikiliwa na Polisi,hata wanaodaiwa kukamatwa hawakuwa wasimamizi wa mitihani.

Nae Mkurugenzi wa shule ya sekondari ya Anderleck Ridges , Alexander Kazimil,  alipoulizwa alisema wanafunzi wake hawana uhusiano na kuibiwa kwa mitihani hiyo,na kukamatwa kwa walimu wake isipokuwa kulikuwa na hila iliyopangwa kuichafua shule yake ili kuharibu sifa iliyojijengea ndani na nje ya nchi.

MKURUGENZI wa Anderlek,Alexander Kazimil.
Kazimil alisema kulikuwa na mpango uliotengenezwa katika mazingira ya  kuiangamiza Taasisi ya Anderlek,kwa kuwatumia mtihani wa historia kwa njia ya simu zao za mikononi,walimu wa shule hiyo ambao hawakuwa wasimamizi ama kuhusika kusogea kwenye kituo cha kufanyia mitihani kisha kutoa ripoti kwa vyombo vya dola.

“Si mwalimu ama mwanafunzi anayehusika,bali kilichohusika ni pesa,lakini napenda kumweleza mtu aliyeandaa mpango huo kuwa pesa sio kila kitu,wakati mwingine pesa hukwama,na mwisho mtu huyo ataumbuka baada ya matokeo kutoka,ninachoomba Baraza la Mitihani lisahihishe mtihani wa somo tunalotuhumiwa kwa umakini mkubwa;mwanafunzi kwa mwanafunzi,swali kwa swali,namba kwa namba,sentensi kwa sentensi na nukta kwa nukta,ili kubaini ukweli wa tuhuma hizo,”alisema Kazimil. 

Hivi karibuni Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga lilidai kuwachunguza walimu wawili wa sekondari hiyo baada ya kupatiwa taarifa kuwa walitumiwa majibu ya somo la historia kwa njia ya simu na mtu mmoja kutoka mkoani Kagera,na kuwachunguza walimu 12 kabla ya kuwashikilia wawili kwa uchunguzi zaidi.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI