MADIWANI
katika Halmashauri ya Mji wa Kahama{CCM}wamepinga Mbunge wa Viti Maalumu mkoa
wa Shinyanga,Salome Makamba{CHADEMA}, kupangwa katika Kamati ya Fedha na
Mipango ya Halmashauri hiyo,huku naye akiwaonya Madiwani kuwa atahakikisha
anatumbua majipu pindi wakiendeleza matumizi mabovu ya fedha za Maendeleo.
Hali
hiyo iliibuka juzi katika kikao cha kwanza cha Baraza la pili la Madiwani wa
Halmashauri ya Mji wa Kahama lenye Madiwani 29,ambapo kutoka upinzani wapo
madiwani wawili tu,kilichokuwa cha kuapishwa,kuchagua Mwenyekiti na kupanga
Kamati mbalimbali ndipo Madiwani hao wa CCM walipoungana kupinga Mbunge huyo
kupangwa Kamati ya Fedha ya Halmashauri hiyo.
Diwani wa viti Maalumu,Aoko
Nyangusu{CCM} alihoji
kanuni iliyotumika kumuingiza mbunge huyo kwenye kamati ya fedha,wakati wabunge wa viti maalumu
hawahusishwi katika Halmashauri zao,mara Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji,Abeli
Shija,alipomaliza kuwatangaza wajumbe wake,huku jina la Makamba likiwemo.
Hoja
iliyoungwa mkono na Madiwani wote watokanao na CCM,huku Diwani wa Kata ya
Mhongolo,Michael Mizubo,akisoma muongozo wa Halmashauri ambao unamtaja Mbunge
wa Jimbo kuwa mjumbe katika Kamati hiyo,ndipo Mkurugenzi Mtendaji wa
halmashauri hiyo,Anderson
Msumba,alipotoa ufafanuzi kipengere kilichotumika
kilifanyiwa marekebisho Bunge lililopita.
“Waheshimiwa
kumbukeni tunaongozwa na Katiba,Sheria za Bunge na Muongozo wa
Halmashauri,vyote tumezingatia katika kumpanga Mbunge huyo,mtambue katika maelekezo ya
sasa lazima awemo diwani wa kutoka vyama vya upinzani,na kwa kuwa
hakuna madiwani wengi wa upinzani na mheshimiwa Makamba anatoka chama cha
upinzani hivyo yuko sahihi kuwemo kwenye kamati hiyo” alisema Mkurugenzi huyo
Hata hivyo madiwani hao hawakuridhika na majibu
hayo huku wakitaka jina la Makamba liondolewe miongoni mwa wajumbe wa Kamati
hiyo,na kumlazimu Mbunge wa jimbo la Kahama,Jumanne Kishimba,kunyanyuka na
kuhoji
sababu ya kumkataa Makamba kama kweli wanadhamira ya kuwatumikia wananchi
kuleta maendeleo,huku akitia shaka kuwa huenda kuna chembe za ufisadi unaowatia hofu
wajumbe ambao walikuwemo
katika Baraza la Madiwani lililopita.
Kwa
upande wake Mbunge wa Viti Maalumu,Makamba{CHADEMA},alishangazwa na misimamo
hiyo ya madiwani na kuhoji katika kamati hiyo kuna nini hadi kumgomea asiwemo,aliwahakikishia kuwa atasimamia maslahi ya Kahama na Taifa kwa
ujumla kwa kufichua ubadhirifu wa fedha za maendeleo hata akiwa nje ya ukumbi
mbali ya kutokuwemo katika Kamati hiyo.
“Nimeshangazwa
na kitendo cha kugoma nisiingie kwenye Kamati ya Fedha na Mipango,hapa kuna kitu huenda mna maslahi
yenu binafsi,lakini naahidi hata mkinikataa
nitafanya kazi ya kamati hiyo nikiwa nje ya kikao,na kwa kuanza napenda Halmashauri
inapatie mchanganuo wa matumizi ya fedha za mrabaha wa Mgodi wa Dhahabu wa
Buzwagi kwa miaka iliyopita,ambako mimi nilikuwa mtumishi,maana natambua kuna
madudu yamefanyika katika fedha hizo” alisema
Makamba
Malumbano katika Baraza hilo lenye Madiwani wa Kata 20,viti
maalumu saba na wabunge wawili,yalihitimishwa kwa Mkurugenzi kuwaahidi
kuwapatia waraka ambao umefafanua juu ya uendeshaji wa Halmashauri,ambao unazingatia Katiba ya nchi,Sheria na
muongozo wa Halmashauri kuwa ni wa tatu,ambao hauwezi kukiuka na kuvunja
maamuzi ya vikao vya Bunge.