
MKURUGENZI wa Hali Halisi Publishers, Saed Kubenea
(kulia) akiwa na Mhariri wa Mwanahalisi, Jabir Idrissa
SAED Kubenea, ameamua kuvunja ukimya baada ya uvumi kuenea kuwa
alikuwa na nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Mafia
mkoa wa Pwani
baada ya kuchukua fomu rasmi kugombea ubunge Jimbo Ubungo. Anaandika Benedict Kimbache. Kubenea ambaye ni Mwandishi Mkongwe wa Habari za Uchunguzi juzi amejizolea umaarufu baada ya kutunukiwa tuzo ya Shujaa kati yetu katika kipengele cha Uwazi na Ukweli na Shirika lisilokuwa la kiserikali la Dream Success Enterprises.
Kubenea ni nani? ni Mwanzilishi, Mhariri Mtendaji
na Mkurugenzi wa Kampuni ya Hali Halisi Publishers Limited(HHPL),
waliokuwa wakichapa gazeti la kufichua maovu la MwanaHALISI na baadae
serikali kulifungia kwa muda usiojulikana.
Kwa sasa baada ya gazeti hilo ambalo lillikuwa likiiumbua serikali kwa maovu yake anamiliki gazeti la mtandaoni la MwanahalisiOnline na MwanaHALISI Forum zenye kauli mbiu ‘Uhuru hauna mipaka’ .
Akizungumza na vyombo vya habari leo mchana makao makuu ya Chama cha
Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ameamua kutoa dukuduku na kusema
“Nimeamua kugombea jimbo la Ubungo ninaamini ni demokrasia na ni haki
yangu kufanya hivyo kama mtanzania” huku akizungumza kwa kujiamini kwa
kurejea kauli ya baba wa Taifa, Mwl. Nyerere aliyesema “wananchi
wanahitaji mabadiliko,wasipoyapata ndani CCM watayatafuta nje ya CCM”.
Kwa vile wananchi wameshindwa kupata mabadiliko ndani ya CCM ,
kubenea amesema ameamua kugombea nafasi hiyo kupitia tiketi ya Chadema,
chama makini, ili aweze kuwa sehemu ya Bunge ya kutunga sheria na
kuisimamia serikali kwa maslahi mapana ya watanzania na ustawi wan chi
kwa ujumla.
Aidha, amesema kwa miaka mingi amekuwa akipambana na ukandamizaji wa
serikali kwa njia ya kalamu kupitia magazeti yake, “nimekuwa nikifanya
shughuli za Bunge nje ya Bunge” amesema sasa kuna umuhimu wa kuwa mbunge
halisi na ninaamini nitakuwa mbunge mzuri na mwenye weledi kuitumikia
nchi yangu kwani nina uzoefu mkubwa wa uendeshaji wa bunge lenyewe,
siendi bungeni kujifunza kanuni za bunge kwani ninajua hata milango ya
kutokea, Kubenea alisisitiza huku akijiamini.
Akizungumza na wanataaluma wenzake amesema binafsi na wadau wote wa
sekta ya habari amefanya kazi kubwa sana ya kutetea vyombo vya habari na
watanzania kwa ujumla, na mpaka kwenye Bunge la 10 alikuwa mmoja wa
wadau waliotumwa kushawishi Bunge kuacha kupitisha Muswada wa Vyombo vya
Habari, ili uweze kujadiliwa kwanza na wadau kitu ambacho kimefanikiwa.
Kubenea amesema angependa kuwa mbunge ili awe mmoja ya wabunge
watakaojadili muswada huo kwa maslahi mapana ya vyombo vya habari.
Moja ya maswali aliyoulizwa waandishi ni pamoja na kutaka kufahamu ni
lini Saed Kubenea alijiunga rasmi na Chadema, alijibu kuwa amejiunga
juzijuzi tu, zaidi ya hayo alisema Katiba ya Chadema ipo wazi kwa
kuruhusu mwananchama kugombea uongozi bila ya kujali alijiunga lini,
kwasababu hiyo yeye anahaki kikatiba kugombea.
Alipoulizwa kwa nini anagombea jimbo la Ubungo amesema ni chaguo lake
kuwakilisha wananchi wa jimbo hilo ili kushirikiana nao kutatua
matatizo yao ya msingi, lakini zaidi anauhakika jina lake likipitishwa
ataweza kugombea jimbo hilo kutokana na makubaliano ya UKAWA.
Alipoulizwa kuwa haoni kuwa kutakuwa na mgongano kati yake na John
mnyika (MB), kwa kugombania jimbo hilo, na kama alishaomba ushauri
kutoka kwa Mnyika, Kubenea amesema haoni tatizo kwani demokrasia
inaruhusu yeyote mwenye sifa kugombea, zaidi ya hayo alisema sio vizuri
kuongea naye kwani yeye ni Naibu Katibu Mkuu(Bara), ana nafasi kubwa
ndani ya chama na yeye ni kiongozi wa wagombea wengine wote, kujadiliana
naye ni kufanya ‘lobbying’, akimaanisha kufanya ushawishi kitu ambacho
sio utawala bora na ni kunyima haki kwa wengine.
Hata hivyo Kubenea alisema akipata fursa atamshauri Mnyika kwenda
kugombea jimbo jipya la Kibamba. Alipoulizwa endapo hataafiki kwenda
Kibamba amesema ataamua kumuachia.
Kuhusu tatizo la maji Kubenea aliulizwa atawezaje kutatua tatizo hilo
kwani Mnyika inaonekana ameshindwa na mpaka sasa kuna kesi inaendelea
huko Bunju, na inaonekana Mnyika ameshindwa kuleta ufumbuzi wa maji
kwani inasemekana kuwa serikali inamkwamisha kwa vile ni mbunge wa
upinzani.
Alijibu kuwa tatizo la maji ni tatizo la kitaifa na wala sio Ubungo
tu, zaidi amesema akifanikiwa kuingia madarakani atafanya uchunguzi
kuona tatizo haswa ni nini, ikiwa ni pamoja na kufahamu je tatizo ni
fedha au ni utendaji? baada ya kufahamu sababu atashirikiana na wananchi
na serikali kuweza kutatua tatizo hilo.
CHANZO CHA HABARI NI MwanaHALISI Online.
CHANZO CHA HABARI NI MwanaHALISI Online.