Na Jackson Bahemu,
Kahama.
WANANCHI wametakiwa kuacha
kulalamikia ucheleweshaji wa hukumu za watuhumiwa wa mauaji ya Albino,badala
yake wawe mstari wa mbele kutoa
ushahidi pindi matukio hayo
yanapojitokeza,hatua itakayosaidia hukumu kutoka kwa wakati.
Rai hiyo ilitolewa na
Afisa Mchunguzi Mkuu,toka Tume ya haki za Binadamu na utawala bora,makao
makuu Dar Es Salaam,Peter Massawe,wakati
wa warsha ya Siku Tatu ya kuandaa
mkakati wa kutokomeza mauaji,ubaguzi na unyanyapaa kwa Albino.
Katika warsha hiyo,iliyoandaliwa
na Shirika la Elimu,Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa “UNESCO”,na
kuwashirikisha wadau mbalimbali,ikiwa na lengo kuu la kushirikisha jamii
kugundua chanzo cha tatizo la mauaji hayo ili kuyadhibiti.
Massawe alisema kuwa jamii
nchini imekuwa hodari wa kulalamika pindi hukumu za watuhumiwa zinapochelewa ama
kutolewa kwa kuwaachia huru,huku ikiwa nyuma katika suala la kujitokeza kutoa
ushahidi wa kuwatia hatiani Watuhumiwa.
“Ili hukumu stahiki na
zinazotarajiwa zipatikane,ni budi tuondoe hofu ya kusaidia polisi,japo inadaiwa
wao ndio chanzo cha kutojitokeza kutoa ushahidi kutokana na usumbufu wao kwa
anaejitokeza kusaidia Polisi,”Alisema Massawe.
Hata hivyo wadau hao
waliitupia lawama serikali kuchelewesha utekelezaji wa hukumu za vifo
zilitolewa kwa waliotiwa hatiani jambo ambalo limesababisha kuendelea kwa
matukio hayo.
Afisa Mtendaji wa Kata ya
Chela,Patrick Mahona,alisema mbali ya serikali kutotekeleza hukumu ya Mahakama
ya kuwanyonga waliotiwa hatiani,ni kiini cha kuendelea kuibuka kwa vitendo
hivyo vya kikatiri.
Aidha alisema hata
mashirika ya haki za binadamu yanachangia kuendelea kuwepo kwa vitendo
hivyo,kwakuwa yamekuwa mstari wa mbele kupinga adhabu ya vifo kwa wanaobainika
na kudhiirika kwa makosa ya mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi.
Akihitimisha warsha hiyo,Afisa
Mratibu wa UNESCO,Mathias Herman,alisema lengo la warsha hiyo,ni kutafiti mbinu
mbadala ya kutowapeleka makambini Albino,kitendo kinachoonyesha ni cha kibaguzi.
Herman alisema UNISCO
imeona vyema kuwafikia wananchi,ili kupanga mkakati utakaonusuru jamii hiyo kuepukana
na ubaguzi,unyanyasaji na mauaji hayo kuendelea ambapo wanatekeleza mradi huo
katika wilaya nne za Kanda ya Ziwa.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI