UCHAGUZI wa Serikali
za Mitaa uliofanyika Jumapili iliyopita na kutawaliwa na dosari
mbalimbali nchini,wilayani Kahama mbali ya kutokea matukio ya kupigwa mabomu ya
machozi na kujeruhiwa kwa baadhi ya wasimamizi wa upigaji kura imelazimika kwa
baadhi ya vituo kurudia uchaguzi.
Katika Halmashauri ya Mji
wa Kahama,ambapo mchuano mkali ulikuwa baina ya Chama Cha Mapinduzi “CCM”na
Chama cha Demokrasia na Maendeleo “CHADEMA”,Chama tawala kimeshindwa kutetea
viti vyake vingi.
Akizungumza na Waandishi wa
Habari ofisini mwake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji wa Kahama;Felix
Kimario,alisema uchaguzi huo uligawanyika
katika maeneo matatu;ya Serikali za Mitaa,Vijiji na Vitongoji.
“Unajua maeneo ya
pembezoni mwa Halmashauri hii bado yana hadhi ya vijiji hivyo ndio maana upo
uchaguzi huo,ambapo tuna vijiji 45,lakini kwa upande wa Serikali ya mitaa kuna
mitaa 32,na vitongoji 218,”Alisema Kimario.
Kimario alisema katika Uchaguzi wa mitaa,Chadema imepata
mitaa 15 huku CCM ikipata mitaa 14, ya Igalilimi,Namanga pamoja na Seeke ambao
walipita bila kupingwa,huku CCM ikiongoza katika ushindi wa Wenyeviti wa Vijiji 40 na Chadema ikipata viti vitano.
Kwa upande wa Vitongoji
218,CCM tayari ina mtaji wa vitongoji 69 waliopita bila kupingwa,huku vitongoji
149 vikiwa vikihakikiwa kura zake kabla ya kutangazwa washindi.
Aidha Mkurugenzi huyo
alisema katika vituo vya Mhongolo na
Mbulu,uchaguzi ulivurugika baada ya kuzuka vurugu za wapiga kura na kusababisha
wasimamizi wawili kujeruhiwa sambamba na
kuharibu pikipiki ya mmoja wa wasimamizi hao,majeruhi hao walipatiwa
matibabu katika hospitali ya mji wa Kahama.
Mkurugenzi wa Halmashauri
ya Ushetu,Isabela Chilumba alisema katika kata 20 zilizopo kata nne za
Kinamapula,Ushetu,Ukune na Chona kuna vituo ambavyo uchaguzi haukuweza
kufanyika kutokana na dosari zilizojitokeza zikiwemo za wagombea kura zao
kugongana.
Alivitaja vituo hivyo kuwa
ni Vijiji vya Hongwa na Butibu katika Kata ya Kinamapula,Vitongoji vya Katule B
na Italike Mashariki vilivyo Kata ya Ukune,pia Kitongoji cha Nsimbo kata ya
Ushetu na Kitongoji cha Usiulize kata ya Chona.Katika Kata ambazo uchaguzi
ulikamilika kura zilikuwa bado zinahakikiwa kabla ya kutangazwa kwa washindi.
Nae Mkurugenzi wa
Halmashauri ya wilaya ya Msalala alisema ni kata sita tu ndizo zilizokamilisha
uchaguzi kati ya kata 18 zilizo katika Halmashauri yake,ambapo ameomba radhi
kwa wananchi ambao Kata zao hazikuweza kufanya Uchaguzi kutokana na dosari
mbalimbali zilizojitokeza ikwemo kuchelewa kufika kwa wakati kwa vifaa vya kupigia
kura.
Alizitaja Kata ambazo
hazikuweza kufanya uchaguzi kuwa ni Isaka,Bulyanhulu,Ngaya,Ntobo
,Bugarama,Ikinda,Bulige,Segese,Mwalugulu,Mega,Mwakata na Kashishi.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI