Sunday, December 28, 2014

KUWASA MATATANI KWA POSHO YA SHILINGI MILIONI 3.6

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO

WAZIRI wa Maji na Umwagiliaji,Profesa Jumanne Maghembe

WAKATI Mzimu wa Akaunti ya Tegeta Escrow ungali ukiitesa Serikali,Wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira katika mji wa Kahama mkoani Shinyanga “KUWASA”wanachunguzwa na TAKUKURU wilayani Kahama,kwa ubadhirifu wa Shilingi Milioni 3.6.


Maamuzi hayo ya bodi ya KUWASA yamewaingiza matatani wajumbe wake baada ya Taasisi ya Kuzuia  na Kupambana na Rushwa Tanzania wilayani Kahama,kuanza kuwahoji juu ya uamuzi huo sambamba na matumizi mabovu ya Madaraka waliyokasimishwa.

Hali hiyo ilibainishwa Desemba 24,mwaka huu katika Ofisi za KUWASA,na Mwenyekiti wa bodi hiyo,Boniphance Lutege wakati akiongea na waandishi wa habari muda mchache mara baada ya  TAKUKURU,kuwahoji na kuchunguza  tuhuma zinazowakabili wajumbe hao pamoja na meneja wa mamlaka hiyo Joel Rugemalila.

Kabla ya hapo mkuu wa TAKUKURU wilaya ya Kahama Enock  Ngailo alisema Taasisi yake inawahoji wajumbe wanane wa mamlaka hiyo kwa tuhuma za maamuzi ya ukiukaji wa sheria na Matumizi mabaya ya bodi hiyo hali ambayo inaweza kuzaa tuhuma zingine wakati wa uchugunzi .

Ngailo alisema mamlaka hiyo inatuhumiwa  kufanya maamuzi bila kufuata kanuni na taaratibu za kisheria kifungu namba 30 cha makosa ya rushwa,ingawa alisema hivi sasa tasisi yake iko katika hatua ya awali ya uchunguzi juu ya Wajumbe wa Bodi ya KUWASA.

Hata hivyo alidai katika uchunguzi kuna mambo mengi yanayoweza kuibuka ikiwemo ubadhirifu wa mali ya umma na mengineyo ingawa Taasisi yake katika hatua ya awali inachunguza tuhuma mbili za Matumizi ya maamuzi ya mamlaka ya kujiongezea posho ya vikao kwa siku bila kufuata taratibu za kisheria na utata wa ajira unao husisha bodi hiyo.


Kufuatia hali hiyo Lutege alikiri bodi yake  kuchuguzwa na TAKUKURU huku akisema kinacholenga wajumbe wake moja kwa moja ni maamuzi ya kupandisha posho ya vikao kutoka shilingi laki tatu  mpaka laki nne na nusu kwa siku huku tuhuma ya ajira akimtupia meneja wake Joel Rugemalila.

Katika hilo Lutege alifafanua,wakati bodi hiyo haijaundwa baada ya iliyokuwepo kumaliza muda wake Rugemalila kupitia uongozi wake waliajiri watumishi wawili katika nafasi za Afisa mahusiano na afisa utumishi bila kupitia bodi kinyume na kanuni na taratibu  za kisheria za ajira

Pamoja na hali hiyo Lutege alisema kwa kuwa tayari swala hilo liko TAKUKURU hivyo ni wajibu wa taasisi hiyo kufanya kazi yake ya uchunguzi na baada ya hapo tuhuma hizo zitabainishwa kisheria

Mamlaka hiyo imekuwa ikikumbwa na kashfa mbalimbali za kiutawala ambapo Taasisi hiyo ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa mara nyingi imekuwa ikiwahoji juu ya tuhuma hizo,lakini inaonyesha haijapa ufumbuzi wa tuhuma za kiutawala za mamlaka hiyo.

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI