KATIKA kutokomeza
ubakaji na mimba za utotoni kwa wanafunzi sambamba na kupata matokeo mazuri ya mwenendo wa kesi wa
vitendo hivyo,Maafisa Watendaji wa kata Wilayani Kahama wametakiwa kuwa mstari
wa mbele kusimamia kesi hizo badala ya
kuwaachia wazazi jukumu hilo.
Agizo hilo
lilitolewa na Mkuu wa Wilaya ya Kahama Benson Mpesya wakati akizungumza na waandishi wa habari
ofisini kwake kuhusu kesi ya mimba inayomkabili Masanja Julius {35}
anayetuhumiwa kumpa ujauzito mwaka 2013 msichana mmoja aliyekuwa mwanafunzi wa
darasa la saba katika shule ya msingi Igwamanoni
B kata ya Bugarama huku kesi hiyo ikionyesha kuwa na mwenendo usioridhisha
toka ifunguliwe.
Mpesya alisema
kuwa Maafisa Watendaji wa kata wamekuwa hawawajibiki vizuri ili kuhakikisha
yanapatikana matokeo mazuri ya mwenendo wa kesi hizo kwa kuwaachia wazazi
jukumu la kufuatilia kesi za Wanafunzi hao zinapotokea huku wakijua kuwa wao
ndio wahusika wakuu wa kusimamia kesi hizo.
Alifafanua kuwa kwa mujibu wa sheria namba 19 ya ubakaji pamoja na ile namba
29 ya Elimu zote zinapinga mimba kwa wanafunzi hivyo kuwaagiza maafisa
Watendaji wa kata kuzitekeleza vyema sheria hizo kwa kuwa wasimamizi waadirifu katika kesi hizo zinawakabili wanafunzi wanapopewa
mimba wakiwa bado shuleni kwa kuzisimamia hadi kuhakikisha zinamalizika kwa
kuleta matokeo mazuri.
Mkuu huyo wa
Wilaya aliwataka Watendaji hao kuongeza hali ya kuthamni Elimu na kuongeza kuwa
kwa kufanya hivyo wanaweza kuisaidia Serikali katika kutimiza malengo yake na
kuwataka kujua suala la kukataa ukweli mahakamani na kupoteza ushahidi
vinaonyesha mianya ya Rushwa kwao.
Kwa upande wake Afisa
Mradi unaowahusisha wanaume na wavulana kushiriki katika kuleta mabadiriko ya
Kijinsia” Man engage”unaofadiliwa na shirika lisilo la Kiserikali la Care
international Gega Bujeja alisema kuwa baadhi ya ya kesi za ujauzito za
wanafunzi nyingi zimekuwa zikiishia njiani hata kama ushahidi wa kutosha upo.
Bujeja aliendelea
kusema kuwa pia kitu kingine kinachosababisha kesi hizo kusuasua ni pamoja na
ushirikinao mdogo baina ya wazazi wa wanafunzi waliopewa mimba sambamba
na waathirika wa suala hilo katika kutoa ushahidi wa kweli pindi wanapotakiwa
mahakamani.
Hata hivyo Afisa
huyo alisema kuwa kwa kupitia mradi huo wa MAN ENGAGE Shirika hilo litaanza
kutoa Elimu kuhusu afya uzazi kwa wazazi katika maeneo mbalimbali wanapofanyia
kazi katika kata za Bugarama, Bulyanhulu na Lunguya hali ambayo inaweza kuleta mabadiliko katika
siku za baadaye.
Katika kikao hicho
kilichojumuisha Waandshi wa habari, Mtendaji wa kata ya Bugarama pamoja na Mratibu
Elimu kata wa kata hiyo kilikuwa na lengo la kutafuta ufumbuzi wa Mwanafuzi
huyo aliyepatiwa ujauzito mwaka jana na Masanja Julius Mkazi wa Igwamanoni na
hivyo kesi hiyo kuonekana kusuasua hali ambayo ilimfanya Mkuu huyo wa Wilaya
kutoa maagizo kwa jeshi la Polisi kutafuta majalada ya kesi hiyo ili yaweze
kupitiwa upya.