Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba amesema Rasimu ya Katiba
iliyopendekezwa na Kamati ya Uandishi ya Bunge Maalumu la Katiba
imeondoa mambo manne muhimu yaliyokuwa kiini cha kupata Katiba ya
mageuzi.
Akiyataja mambo hayo muhimu ambayo ni maadili ya
viongozi wa umma, madaraka ya wananchi, mgawanyo wa madaraka na
muungano. “Tutakutana mtaani. Tume tutaendelea kutetea rasimu yetu na
wao wawaeleze wananchi kwa nini wameondoa maoni yao yaliyokuwa katika
Rasimu ya Pili ya Katiba,” aliongeza kwa ufafanuzi Jaji Warioba.
Akizungumza katika maadhimisho ya miaka 19 tangu
kuanzishwa kwa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Dar es Salaam
jana, Jaji Warioba alisema rasimu hiyo inatofautiana kwa kiasi kikubwa
na rasimu iliyotolewa na tume hiyo Desemba mwaka jana.
“Sina hakika kama tutapata Katiba Mpya labda
Katiba iliyoboreshwa. Rasimu au Katiba itakayopendekezwa na Bunge
Maalumu haitapigiwa kura hadi 2016. Sina hakika kama kura hiyo itapigwa
kwa kuwa hakuna maridhiano hasa kuhusu muungano, rasimu hiyo itaanza
kupingwa tangu siku ya kutolewa kwake,” alisema.
Aliongeza, “Wakati wa kampeni za uchaguzi mwaka
kesho Katiba Mpya itakuwa agenda, na agenda hiyo inaweza kuigawa nchi.
Kuna uwezekano mkubwa kwamba mwaka 2016 badala ya kupiga kura mchakato
ukaanza upya.”
Jumatano wiki hii Mwenyekiti wa kamati hiyo,
Andrew Chenge aliwasilisha rasimu hiyo bungeni na kueleza kuwa kamati
yake imefuta ibara 28 zilizokuwa katika rasimu ya Jaji Warioba na kuacha
ibara 47, kuongeza ibara 42 na kurekebisha ibara 186.
Alisema rasimu hiyo ina sura mpya mbili ambazo ni
Mamlaka na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na nyingine inayohusu Ardhi,
Maliasili na Mazingira ambayo haikuwekwa katika rasimu ya Warioba kwa
kuwa si mambo ya muungano.
Rasimu hiyo ilirejesha muundo wa Serikali mbili
kama ilivyo sasa na kutupilia mbali muundo wa Serikali tatu
uliopendekezwa na Tume ya Jaji Warioba.
Huku akiwa makini, Jaji Warioba ambaye alitumia
saa 1:02 kufafanua umuhimu wa mambo manne yaliyoachwa katika rasimu
iliyotolewa na Bunge la Katiba, alisema hivi sasa wajumbe wa Bunge la
Katiba wana msemo wao kuwa “Warioba ni shida”, kufafanua kuwa
watakapomaliza vikao vya Bunge hilo Oktoba 4, mwaka huu na kurejea
mtaani walipo wananchi ndiyo watajua nani ni ‘shida’, kati yake na wao.
Akizungumzia kitendo cha Bunge hilo kubadili
kanuni ili kuruhusu wajumbe wake kupiga kura za kupitisha rasimu hiyo
kwa baruapepe (e-mail) na nukushi (fax) wakiwa nje ya nchi, Jaji Warioba
alisema, “Utaratibu huu hauwezi kutuletea Katiba ya maridhiano. Hata
mimi nimeanza kukata tamaa.
Huku akishangiliwa kila mara na mamia ya watu
waliohudhuria kongamano hilo, wakiwamo wasomi na baadhi ya waliokuwa
wajumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Warioba alisema kila
mjumbe wa tume hiyo alikuwa na mawazo yake juu ya Katiba, lakini
waliweka kando mawazo yao baada ya kusikia kauli za Watanzania juu ya
Katiba wanayoitaka.
Katika maadhimisho hayo, Jaji Warioba pia
alizindua kitabu cha marehemu Dk Sengondo Mvungi kiitwacho ‘Mvungi
anapumua Katiba’. Dk Mvungi aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Katiba na mmoja
wa waanzilishi wa LHRC, alifariki dunia mwaka jana nchini Afrika Kusini
alikopelekwa kutibiwa baada ya kujeruhiwa na majambazi akiwa nyumbani
kwake.
Chanzo cha Habari ni Gazeti la Mwananchi.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI
Chanzo cha Habari ni Gazeti la Mwananchi.