MWITO
umetolewa kwa wananchi wa Kata mbalimbali katika Jimbo la Kahama kuwazomea
madiwani wazembe ambao hawawaletei maendeleo ipasavyo ambayo yapo chini ya uwezo
wao.
Mwito
huo ulitolewa juzi na Mbunge wa Jimbo la Kahama James Lembeli kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye mtaa wa
Mayila katika Halmashauri ya Mji wa Kahama ambapo alisema ili kuleta changamoto
ya uwajibikaji kwa madiwani wazembe wanapaswa kuwazomewa.
Lembeli alitoa wito huo kutokana na wananchi wa eneo la Mayila kutoa malalamiko juu ya
ubovu wa barabara katika mtaa huo ambao
walisema tangu miaka 17 iliyopita eneo hilo halijawahi kufanyiwa matengenezo ya
miundo mbinu hiyo.
Alisema suala la utengezaji wa barabara hiyo ni mpango wa
Bajeti unaopangwa na Madiwani wa Halmashauri ya Mji hivyo kukosekana kwa
matengenezo kunaashiria ni uzembe unaofanywa na diwani wao hivyo ikibidi azomwe
ili apate msukumo wa kuwajibika.
Lembeli alisema pamoja na
mambo makubwa aliofanya Diwani wa eneo hilo Amosi Sipemba lakini si mwisho wa
kuleta maendeleo mengine ambayo yapo chini ya Halmashauri ya Mji na yeye ni
diwani anayehudhuria vikao vyote vya maamuzi.
“Mtambue jimbo lina Kata 34,msaada wangu wa kubaini
changamoto zilizopo ni Diwani,kama yamemshinda ni budi anifikishie nami nitaenda kusukuma huko Halmashauri,”Alisema
Lembeli.
“Mkiona bado mambo hayaendi ikibidi mzomeeni ili akamueleze
mke wake,kama mimi nilivyozomewa mwaka 2007 mbele ya Rais nilijifunza mengi sana
na leo hii siwezi kuzomewa tena,hivyo nae akipata changamoto hiyo
atawajibika,”Aliongeza Lembeli.
Hata
hivyo kabla ya hapo Diwani wa Kata ya Nyihogo katika eneo hilo Sipemba alisema
tangu aingie mwaka 2010 hakukuwa na barabara yoyote iliyochongwa katika eneo
hilo lakini mpaka sasa asilimia kubwa zimefanyiwa matengenezo.
Akizungumzia kuhusu kuzomewa na wananchi Sipemba alisema
yeye sio mhandisi wa kutengeneza barabara isipokuwa na yeye huenda kuomba msaada
katika Halmashauri pamoja na misaada mingine kutoka kwa Mbunge
huyo.
Lembeli yupo ziara katika jimbo lake ambapo katika Kata ya
Nyihogo pamoja na mambo mengine kuombwa na Diwani huyo alichangia mabati 60
kwenye Shule ya Msingi Kilima B pamoja na Shilingi Milioni Mbili na Nusu kwa
ajili ya gati la maji ya ziwa Victoria kwa wananchi wa mtaa wa
Mayila.