Watafiti
katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba cha Temple, Marekani wamegundua dawa ya
kuangamiza Virusi Vya
Ukimwi (VVU) ambayo ni ya uhakika zaidi ukilinganisha na
zilizowahi kupatikana katika tafiti za awali duniani.
Dawa
yao inaweza kutumika kwa tiba ya wanaoishi na VVU na kinga kwa wale ambao bado
hawajaambukizwa.
Mmoja
wa watafiti hao, Dk Kamel Khalili aliwaambia waandishi wa habari juzi mjini
Philadelphia, Marekani kuwa tofauti na utafiti mwingine, wao wamegundua namna
ya kukiondoa kirusi kilichoingia kwenye kinasaba (DNA) ndani ya CD4 na kukitoa
nje na hatimaye kukiua.
Alisema
dawa hiyo inafanya kazi hiyo bila kuathiri seli za mwili wa binadamu.
Dk
Khalili alisema ugunduzi wao ni wa hali ya juu zaidi kwa sababu teknolojia ya
kutengeneza dawa hiyo ni tofauti na nyingine zilizokwisha kugunduliwa ambazo
hazina uwezo wa kupenya ndani ya seli za binadamu, bali kuathiri tu VVU
vilivyopo nje yake, ndani ya mfumo wa damu.
“Dawa
yetu inakivuta kirusi nje ya seli (CD4) bila kuiathiri seli yenyewe na kukiua.
Hivyo dawa hii itatumika kwa muda fulani na kuua virusi vyote mwilini na hakuna
haja ya kuitumia wakati wote kama ilivyo dawa ya kufubaza VVU (ARV).”
ARV
huangamiza VVU vilivyopo kwenye damu na kuendelea kuviacha hai vile ambavyo
tayari vimeingia ndani ya CD4, hivyo kufanya virusi kuzuka upya pindi
mwathirika anapoacha kutumia dawa.
Mmoja
wa wataalamu katika Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu Kituo
cha Mbeya (NIMR-MMRC), Clifford Majani ameuelezea utafiti huo kama mwanga mpya
katika teknolojia ya kukabili VVU.
“Kama
imepatikana teknolojia ya kukiondoa kirusi ndani ya seli ni hatua nzuri ya
kukabili VVU. Hili lilionekana kuwa gumu mwanzoni,” alisema Majani.
Alisema
imekuwa vigumu kuua kirusi kikiwa ndani ya seli na hata baadhi ya wanasayansi
wamejaribu kutengeneza dawa itakayotambua seli zilizoathirika ili ziuawe lakini
hilo likawa gumu.
“Inaweza
ikapatikana dawa ya namna hiyo (inayoua seli zilizoathirika) lakini ikawa
inaathiri vitu vingine ndani ya mwili.
"Hilo halikubaliki. Kikubwa katika ugunduzi huo ni dawa kuweza kukifuata kirusi kinakojificha na kukiondoa, jambo ambalo dawa nyingi zimeshindwa zikiwamo ARV,” alisema.
"Hilo halikubaliki. Kikubwa katika ugunduzi huo ni dawa kuweza kukifuata kirusi kinakojificha na kukiondoa, jambo ambalo dawa nyingi zimeshindwa zikiwamo ARV,” alisema.
Hata
hivyo, Majani alisema changamoto ambayo inaweza kujitokeza katika majaribio ya
dawa hiyo ni usalama wakati wa matumizi.
“Lazima
dawa hiyo ichunguzwe isije ikawa inaathiri viungo vingine pamoja na utendaji wa
mwili kwa ujumla. Maana hapo ndipo dawa nyingi zinaposhindwa… Tusubiri tuone
hii inaweza kuwa na matumaini zaidi,” alisema Majani.
Mkutano
wa Ukimwi
Ugunduzi
huo umekuja wakati wanasayansi, waunda sera na wadau wa mapambano ya VVU wakiwa
wanatoa kauli za kukata tamaa kwenye mkutano wa Ukimwi unaomalizika kesho huko
Melbourne, Australia.
Wanasayansi
kadhaa wanaotoka kwenye taasisi kubwa za utafiti za VVU wameweka wazi kuwa
tafiti nyingi zilizokuwa na matumaini zimeshindwa kufanya kazi kwa asilimia 100
baada ya dawa zake kufanyiwa majaribio kwa sababu dawa zake zinapotumika,
vipimo huonyesha wamepona lakini baada ya muda VVU hurejea upya.
“Kinachoonekana
ni kwamba virusi hivi hujificha sehemu fulani ya mwili ili visiathirike na
kusubiri mtu aache dawa ili virejee upya kushambulia CD4,” alisema Mkurugenzi wa
Taasisi ya Utafiti ya wa Magonjwa ya Kuambukiza na Kinga ya Peter Doherty ya
Australia, Profesa Sharon Lewin.
Dawa
mpya inavyofanya kazi
Dk
Khalili alisema wametengeneza dawa yao kwa protini maalumu ambayo inakata
sehemu ya seli iliyoshambuliwa na kirusi cha Ukimwi na kukivuta nje.
Baada
ya kukivuta, dawa huachana na seli hiyo na kuiacha ikijitibu yenyewe na kupona
kabisa kiasi cha kuendelea na kazi zake za kinga mwilini mwa binadamu bila
tatizo.
VVU
kwa kawaida hushambulia seli kinga aina ya CD4 na kuzifanya kama kiwanda cha
kuzalishia virusi vingine.
Kwa
kawaida seli ikishaingiliwa na kirusi, huacha kazi yake ya kinga ya mwili na
badala yake kuchukua jukumu la kutengeneza VVU.
“Dawa
yetu inafanya kazi kwa haraka, kwa makini na bila kuathiri seli,” alijigamba Dk
Khalili.
Alisema
tayari imefanyiwa majaribio maabara na kuonekana inafanya kazi vizuri na sasa
wamehamishia majaribio kwa wanyama.
Katika
maabara, alisema dawa hiyo ilifanyiwa majaribio kwa damu ya binadamu na
ikaonyesha kufanya kazi kwa asilimia 100.
Dk
Khalili anaamini kwamba majaribio hayo yatawachukua miaka michache...
“Lakini tunaamini ni mfumo ambao utaweza kufanya kazi vizuri kwa binadamu.”
Alisema
wanachofanya sasa ni kuangalia mfumo ambao utakuwa mzuri zaidi kwa ajili ya
tiba ya binadamu.
Kwa
namna teknolojia ya dawa hiyo ilivyo, alisema wanaweza kuitumia kwa ajili ya
kuwatibu wale ambao tayari wameambukizwa na hata kuwakinga wale ambao siyo
waathirika.
Uzuri
wa dawa hiyo, pia alisema inaweza kutumiwa na mtu ambaye anatumia ARV pasipo
kuingiliana kiutendaji.
Ugunduzi
wao ulichapishwa kwenye Jarida la Taifa la Elimu ya Sayansi la National Academy
of Science la Marekani na kuonekana kuvuta hisia za wengi.
Hali
ya Ukimwi duniani
Akizungumza
kwenye mkutano wa Melbourne, Profesa Lewin alisema tafiti za sasa zinaonyesha
kuwa karibu watu milioni 14 duniani wanaishi na VVU.
Alisema
mamilioni ya watu hao wamekuwa wakisaidiwa kwa kutumia ARV, wakati huu ambao
bado hakuna kinga wala tiba, inayoaminika.
Alisema
ingawa tafiti nyingi hazijaonyesha matumaini waliotarajia ya kupata kinga na
chanjo, bado juhudi zinaendelea ili kuhakikisha wanafikia mahali HIV inakuwa
haina nafasi katika mwili wa mwanadamu.
Alisema
pamoja na matokeo hasi ambayo yamejitokeza kwenye tafiti nyingi, bado anaamini
kwamba ipo siku chanjo na tiba vitapatikana.
Wanasayansi
waliohudhuria mkutano huo waliitaka dunia isiogope kutokana na kushindwa kwa
baadhi ya tafiti kama ilivyokuwa kwa mtoto wa Jimbo la Mississippi, nchini
Marekani ambaye alitangazwa amepona na baadaye virusi vikaibuka upya.
Chanzo:Gazeti la Mwananchi