MKUU wa wilaya ya Kahama;Benson Mpesya akisisitiza jambo.
WAFANYABIASHARA
ndogo wanaofanya shughuli zao hizo katika masoko yasiyo rasmi katika
Halmashauri ya mji wa Kahama wametakiwa kuondoka mara moja na kuhamia
eneo
rasmi kabla hawajaondolewa kwa nguvu katika Oporesheni inayoendelea Mjini
Kahama.
Agizo hilo
lilitolewa juzi na Mkuu wa wilaya ya Kahama Benson Mpesya wakati alipotembelea
na kuongea na wafanyabiashara wa soko jipya la Mayila lililopo Kata ya Nyihogo,na
kuwaeleza changamoto zilizopo katika eneo hilo kuwa zitashughulikiwa kwa
wakati.
Mkuu huyo
wa wilaya alisema anatambua changamoto zilizopo sokoni hapo zikiwemo za miundo
mbinu za barabara za kufika hapo hata hivyo alibainisha si kigezo cha kuanzisha
masoko yasiyo rasmi kwakuwa serikali haina utaratibu wa kila mtu kuanzisha soko
lake kadri anavyotaka mwenyewe.
Mpesya
alisema Halmashauri ya Mji tayari ina maeneo ambayo imejenga masoko ambayo
kuwepo kwake kwa Wafanyabiashara hao kuwataka kuhamia katika maeneo hayo rasmi
hatua itakayosaidia utunzaji mzuri wa usafi wa mji na upatikanaji wa ushuru
unaosaidia maendeleo ya Mji.
Hivyo
aliwaomba wananchi kumpatia orodha ya masoko yasiyo rasmi ikiwemo soko la kwa
Mlapa lililopo kati ya Kata za Mhungura na Nyihogo ambayo licha ya wafanyabiashara
wake kuondolewa wameanza kurudi na kuhadharisha kuwa wanaoendelea kukiuka
taratibu pindi watakapokamatwa katika maeneo hayo wakifanya biashara
watachukuliwa hatua kali za kisheria.
Kabla ya
hapo Wafanyabiashara hao walimueleza Mkuu huyo wa wilaya kuwa wanashindwa
kulipa ushuru katika Halmashauri ya Mji kutokana na biashara zao kuathiriwa na
uanzishwaji wa masoko holela mitaani hali ambayo Mpesya amesema watu hao
watakumbwa na oporesheni hiyo inayoshirikisha pia Jeshi la Polisi.
Kwa upande
wake Diwani wa Kata ya Nyihogo Amosi Sipemba alisema wafanyabiashara hao
wamewekeza zaidi ya Shilingi Bilioni Tatu katika soko hilo la Mayila ili
serikali iweze kunufaika ni budi masoko ya mitaani yaondolewe hali ambayo Mkuu
huyo wa wilaya amesema wataondolewa na kutakiwa kuhamia soko la Mayila.
Akizungumzia
soko la Wakulima Mkuu huyo wa wilaya alisema Wafanyabiashara katika eneo hilo
lazima waondoke baada ya kukamilika kwa soko la Majengo kwakuwa eneo hilo
Serikali hainufaiki na chochote wakati ikitumia gharama kubwa kusomba
mrundikano mkubwa wa taka unaozalishwa toka ndani ya soko hilo.
|