MASKINI Mtoto Neema Joseph { 2 }muda wote kwake ni kilio kutokana na maumivu yanayomkabili,hapa akiwa mgongoni mwa mama yake mzazi;Annastazia Yohana {28}. |
MTOTO Neema Joseph {2}akilia kwa uchungu kutokana na mateso anayopata. |
MTOTO Neema Joseph {2}akilia kutokana na mateso ayapatayo. |
MKURUGENZI wa HUHESO FOUNDATION;Juma Mwesigwa akiwashukuru akina mama ambao waliguswa na mateso apatayo mtoto Neema Joseph {2}na kuamua kumchangia fedha za kujikimu. |
MAMA mzazi wa mtoto Neema Joseph {2}katikati aliyejifunika kichwani kitenge kumkinga mwanaye na jua,akiambatana na wasamaria wema watatu wakitoka uwanja wa michezo wa Halmashauri ya Mji wa Kahama. |
YARABI Maskini!Mtoto Neema
Joseph {2}anateseka kwa maradhi ya jicho ambalo limefumuka na kutoka nje huku
likitoa harufu kali,huku akilia kila mara bila shaka kutokana na maumivu yasiyomithilika.
Mtoto huyo ambaye
anaendelea na mateso ya maradhi ya jicho huku hatima yake ikiwa haijulikani
anaishi na mama yake mzazi;Annastazia Yohana{28} katika kijiji cha Bugomba Kata
ya Bulungwa wilayani Kahama, anaomba msaada utakaomuwezesha kufanyiwa matibabu
katika hospitali za Rufaa.
Akiomba msaada kwa niaba
ya mwanaye huku akibubujikwa na machozi pengine kutokana na mateso ayapatayo
binti yake,mama mzazi wa mtoto huyo alisema hali ya maisha yake kiuchumi si
nzuri hasa baada ya kufiwa na baba wa mtoto huyo miezi tisa tangu amejifungua,na
kumuachia watoto wengine wawili.
Alisema tangu kipindi
hicho amekuwa na maisha ya shida kutokana na kutokuwa na msaada kutoka kwa
ndugu yake ama upande wa mume wake kutokuwa na hali nzuri ya kimaisha hivyo
kutokuwa tayari kumsaidia kubeba mzigo wa maisha yake.
Akizungumzia ugonjwa wa mwanae,alisema
ulianza mwezi mmoja uliopita ambapo tatizo lilianza kwa jicho hilo la upande wa
kulia kuwa jekundu huku likibubujikwa na machozi ya mara kwa mara.
“Hali iliyojitokeza iliambatana
na kulifikicha jicho kitendo kilichonipa hisia kuwa
mwanangu anapata mateso,hima nilimpeleka kituo cha afya cha Kata yangu ambapo
alichunguzwa na kupatiwa matibabu,ambayo hayakumpatia ahueni yoyote.”Alisema bi
Annastazia.
Alisema baada ya kuona
hali inazidi kuwa mbaya huku jicho likipasua na kutokeza kwa nje kiasi cha
kutisha alishauriwa na baadhi ya watu kuwa tatizo hilo litakwisha pindi
akimpeleka hospitali ya Nkinga.
“Nilipopata ushauri
huo,huku nikionyeshwa mmoja wa wanakijiji ambaye mwanae alitibiwa
huko,nilimfuata mama yangu mzazi na kumuomba aniangalizie wanangu wawili ambao
mpaka sasa anao,niliuza akiba yangu yote ya chakula ili kupata pesa ya nauli na
matibabu.”Alisema mama wa mtoto huyo.
Mama huyo alisema kuwa
baada ya madaktari wa hospitali ya Nkinga kumuona na kumfanyia uchunguzi
walimueleza tatizo la mwanae linaweza kutibiwa hospitali ya rufaa ya Kilimanjaro
Christian Medical Center “KCMC” ya Moshi,na kulazimika kurejea nyumbani kwakuwa
hakuwa na uwezo wa kufika huko.
Aliendelea kusema hali ya
mwanae ilizidi kuwa mbaya hasa jicho la mwanae kuzidi kutoka nje huku likiambatana
na majimaji ya njano sambamba na mtoto kulia kwa maumivu,hivyo bibi mzazi wa
mtoto huyo ambaye ni mama yake Annastazia alitoa sehemu ya mazao yake na kuuza ili
kupata nauli ya kufika Kahama,kuomba msaada wa matibabu.
“Mjini Nilikutana na
wanawake watatu ambao walionieleza nifike uwanja wa michezo kuna madaktari wa
saratani walioletwa na Shirika moja ili wamchunguze mwanangu,tulipofika
tulielekezwa tumuone mkurugenzi wa Shirika hilo”Alisema mama huyo.
Akiwa katika uwanja huo
kwa msaada wa Mkurugenzi wa Shirika la The Foundation for Human Healthy Society
“HUHESO FOUNDATION”lenye makao yake makuu wilayani Kahama,liliendesha harambee
la kumsaidia kupata fedha za kujikimu na kufanikiwa kupata kiasi cha Shilingi
80500/=.
Kwa upande wake Mkurugenzi
wa Shirika la HUHESO FOUNDATION;Juma Mwesigwa ambalo kwa kushirikiana na
Hospitali ya wilaya ya Kahama lilikuwa likiendesha upimaji wa saratani ya
shingo ya uzazi,alimpokea mama huyo na mwanae na kwenda kumkabidhi kwa Kaimu Mganga
Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama.
Nae Kaimu Mganga Mkuu wa
hospitali ya wilaya ya Kahama;Dk.Helen Yesaya,alikiri kumpokea na mtoto huyo na
kumpatia uchunguzi wa awali uliobaini kuwa ana tatizo la saratani ya jicho
hivyo kumfanyia utaratibu wa kumpeleka hospitali
ya rufaa Bugando kwa ajili ya matibabu zaidi.
Akizungumzia taarifa hizo
mama wa mtoto huyo alisema hali yake kiuchumi ni mbaya,uwezo wa kuishi jijini
Mwanza wakati mwanae akiendelea na matibabu hana na ana mashaka kama atapata
matibabu stahiki kutokana hana fedha,hivyo anaomba achangiwe fedha ambazo
anaamini zitakuwa msaada wa kupata tiba bora ya mtoto wake.
Kutoa ni moyo!Kwa yeyote
aliyeguswa na tatizo la mtoto huyu anaweza kumsaidia kwa kuwasiliana na Shirika
la HUHESO FOUNDATION la mjini Kahama kwa namba 0753 444 840.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI