WASIWASI wa alama za nyoka
wawili waliopo kwenye lango la kuingilia katika hospitali ya wilaya ya Kahama
mkoani Shinyanga,umekuwa sababu ya kuwatia hofu baadhi ya wagonjwa
wanaoingia kutibiwa kwa imani ya kunyonywa damu.
Katika madai yao kwa nyakati
tofauti jana waliotoa kwa waandishi wa habari baadhi ya wakazi wa wilaya ya
Kahama walisema wamekuwa na hofu kubwa pindi wanapougua kwenda katika hospitali
hiyo hasa wenye matatizo ya upungufu wa damu.
Hospitali hiyo ya wilaya kwenye
lango kuu la kuingilia imedaiwa kuna alama ya nyoka wawili ambao baadhi ya
wananchi hao wameingiwa na imani ya kudai ni alama ya freemasons ambayo ni
imani ya kishetani inayotamba hapa duniani.
Walidai hofu zaidi inayowatawala ni
kwa wagonjwa wenye matatizo ya kuishiwa damu mara kwa mara ambao
wameingiwa na imani kwamba nyoka hao huwanyonya damu huku wakipendekeza alama
hizo ziondolewe kwenye lango hilo.
Hata hivyo Mganga Mfawidhi katika
hospitali hiyo Dk.Joseph Fwoma alisema alama hizo siyo nyoka kama wanavyodai
bali ni mnyoo wa kwanza kwa binadamu ambao hutumika katika baadhi ya hospitali
nyingi duniani.
Fwoma alisema alama hiyo ndiyo nembo
iliyosababisha kuwepo kwa madaktari duniani kwakuwa ndiyo mnyoo wa kwanza
kutibiwa na daktari na ndiyo ishara ya kuwepo kwa hospitali.
Hospitali ya wilaya ya Kahama
inahudumia wagonjwa zaidi ya mia saba kila siku huku wengi wao wakiingia
kutibiwa kwa madai ya hofu ya kunyonywa damu na nyoka waliochorwa kwenye
lango la kuingilia.