CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo
“CHADEMA”wilaya ya Kahama,kimetoa siku 14 za kujieleza kwanini wasifukuzwe
uanachama Diwani wa Kata ya Majengo;Bobson Wambura na viongozi wawili wa
chama hicho kwa utovu wa nidhamu na kutowajibika.
Akizungumza na waandishi wa Habari
kwenye ofisi za chama hicho wilaya,Mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Kahama;Juma
Ntahimpera,alisema uamuzi huo umefikiwa na Baraza la Mashauriano la wilaya
lililokutana hivi karibuni baada ya kuamua kuwajadiri viongozi hao watatu
kutokana na mwenendo wao ndani ya chama kukiuka maadili,kanuni na katiba ya
chama hicho.
Alisema pamoja na mambo mengine
lilijadiri mwenendo wa Diwani huyo ambaye mara nyingi amekuwa akikashifu chama
kuwa hakina mchango wowote na wadhifa alionao ambao ameupata kutokana na
umaarufu alionao katika jamii na si kwa nguvu ya chama.
Alisema baraza hilo lilishangazwa na
hatua ya diwani huyo kudharau maamuzi ya kamati kuu ya kumvua madaraka Zitto
Kabwe kwa kuendelea kuimuita Naibu Katibu Mkuu na kudai yuko tayari kukihama
chama kwakuwa kimemuonea katika mkutano wa hadhara wa Katibu Mkuu wa CHADEMA
Taifa;Dr.Willibroad Slaa.
Aidha Baraza hilo limeamua kuchukua
hatua hiyo kwa diwani huyo kutokana na kudharau ulinzi wa chama uliokuwa katika
mkutano wa Dr.Slaa kwa kwenda na walinzi wake mwenyewe ambao walivuruga ulinzi
wa chama mkutanoni hadi busara ilipotumika ili kuweka mambo sawa.
Kwa upande wa viongozi wawili
aliowataja kuwa ni Mratibu wa Vijana wa wilaya wa chama hicho;Vicent
Manyambo,tuhuma zake ni kuiba nyaraka za chama ofisini,kutapeli fedha kwa
kutumia nembo ya chama sambamba na kuwashitaki baadhi ya viongozi wenzake
polisi katika masuala yanayohusu chama pasipo kutoa taarifa katika chama.
Pia alimtaja Katibu wa Jimbo la
Kahama;Vicent Kwilukilwa kukumbwa na fagio hilo kutokana na kutoa siri za chama
katika vyombo vya habari pasipo kuagizwa na kikao chochote halali sambamba na
kutuma ujumbe mbalimbali kwa njia ya maandishi ya simu yenye lengo ya kuleta
vurugu ndani ya chama.
Hata hivyo Ntahimpera aliwaomba
wanachama na wapenzi wa CHADEMA kuwa na subira hadi siku hizo ziishe ili wapate
majibu yao,ambapo kikao cha baraza kitaketi na kutoa maamuzi yanayozingatia
maelekezo kutoka ndani ya Katiba ya Chama kisha watafahamishwa hatua
zitakazochukuliwa juu ya viongozi hao.