M
|
uasisi wa Chama cha Kutetea Haki na
Maslahi ya Walimu Tanzania ( CHAKAMWATA ),Mkoani Shinyanga,Mwalimu Lawrance
Mbaga,ameuvunja uongozi wa chama hicho baada ya
kubaini hakijajikita kutetea
maslahi ya walimu na kurejea chama chake cha zamani cha CWT.
Mbaga ambaye alikuwa Katibu wa CHAKAMWATA,Mkoa
wa Shinyanga,pia akitumikia wadhifa huo ngazi ya wilaya ya Kahama,aliuvunja
uongozi na kukabidhi nyaraka zote za chama hicho kwa uongozi wa Chama cha walimu (CWT ) wa wilaya ya Kahama,katika
kikao kilichofanyika katika ofisi za CWT wilayani Kahama.
Alisema kisheria ana nguvu ya kuvunja
uongozi huo kwakuwa ndiye aliyeuteua tena kwa kuzingatia urafiki,pasipo
kuzingatia kikao ama mkutano wowote na kuwapangia mamlaka ya kuongoza kwa
nyadhifa zile zile kuanzia ngazi ya wilaya hadi Mkoa.
Mbaga ambae ni mwalimu wa Shule ya
Msingi Masabi katika Halmashauri ya Msalala wilaya ya Kahama alisema ameamua
kuvunja uongozi huo,baada ya kubaini uwepo wake umekuwa sababu ya kuwagawa na
kuvunja umoja na mshikamano katika kutetea maslahi ya walimu pamoja na kutatua
changamoto zinazowakabili.
Alidai kubaini CHAKAMWATA hakipo kwa
ajili ya kutetea maslahi ya walimu bali ni kupinga chama kilichopo cha
CWT ambacho kina malengo sahihi kwa walimu huku kikiwa kimeishafanya mambo
mengi mazuri yenye kutatua changamoto zinazowakabili katika majukumu yao.
“CHAKAMWATA walinirubuni nilipokuwa
likizo nyumbani Mbeya,viongozi wa chama hicho wana tatizo la ueneo,kutokea
kwangu Mbeya ndiyo ilikuwa sifa ya kupata nafasi hiyo,ntahakikisha wanachama
wachache niliowalaghai ninawarejesha CWT,”alisema Mwalimu Mbaga.
Aidha alitumia fursa hiyo kuwaasa walimu
wenzake kutohadaika na kuanzisha vyama vingine vinavyokinzana na CWT,ambavyo
vinakuwa sababu ya migongano isiyo na tija katika umoja na mshikamano wao ambao
ndio silaha kubwa ya kutetea maslahi yao.
“Mshikamano ndiyo ukombozi wa
wafanyakazi kitendo cha kuanzisha chama kingine cha walimu ni kuwagawa na
kumomonyoa nguvu na mshikamano wa walimu ndiyo maana tumeamua kuivunja
CHAKAMWATA na kurudi CWT ,, Alisema Mbaga.
Mwenyekiti wa CWT wa wilaya ya Kahama
,Edina Kalambo,alipongeza maamuzi ya muasisi wa CHAKAMWATA wilayani Kahama na
mkoani Shinyanga, kujiondoa katika chama hicho, kwa sababu kilichopo cha CWT
kipo imara katika kutatua changamoto za walimu zinazowakabili.
Mwalimu Kalambo aliwakumbusha kwamba
CWT ipo kwa ajili ya kutetea maslahi mapana ya walimu na kuwataka kuacha
kugawanyika bali waendeleze umoja wao na mshikamano hatua itakayowasaidia
kuwafikisha mbali ya kiuchumi na taaluma yao.
Nae Katibu wa CWT wa wilaya ya Kahama
Dauda Mohammed Bilikesi,alionya tabia ya kuanzisha utitiri wa vyama,ambavyo
vinaweza kuwa sababu kudhoofisha nguvu ya CWT ambacho hata hivyo alijinasibu kuwa
kipo imara na kinawajibika ipasavyo kutetea stahiki
za walimu.
Kwa upande wake mwenyekiti wa CWT wa
mkoa wa Shinyanaga George Nyagusu alisema viongozi walioanzisha chama hicho
kipya cha CHAKAMWATA ambacho makao yake makuu yapo mkoa wa Mbeya na
walioanzisha ni baada ya kukosa nafasi za uongozi katika chaguzi za CWT za
taifa.
Alitoa wito kwa walimu kujiunga na
chama chao cha CWT kwa sababu kipo imala , kutetea maslahi yao na kuwataka
wasigawanyike na kuendekeza kuanzisha vyama vipya na kuwaomba walimu wote
nchini kutimiza wajibu wao kabla hawajadai stahiki zao.
CHAKAMWATA kilianzishwa na kupata usajiri wake
Machi 18 , 2015 kikiwa na Makao Makuu yake mkoani Mbeya na kilimteua Mbaga kuwa
katibu wa mkoa wa Shinyanga na kuunda uongozi ambao kwa pamoja wameamua kujivua
madaraka hayo na kurejea CWT.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI