Wednesday, August 23, 2017

WACHEZAJI,BENCHI LA UFUNDI SIMBA AMA YANGA NANI KUANGUKIWA JUMBA BOVU LEO?

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO




M
abingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara,Yanga African na watani zao wa Jadi,Simba Sport Club,wanateremka dimbani leo kumenyana kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii,ambao ndio ufunguzi wa Msimu Mpya wa Ligi Kuu mwaka 2017/2018.



Pambano hilo la Watani wa Jadi,kwa historia ya timu hizo humalizika kwa timu inayopoteza mchezo kutoyakubali matokeo kimchezo,kwa mkasa wa kutimua benchi la ufundi pia kuibua hujuma kwa baadhi ya wachezaji ama viongozi wa timu.

Katika pambano hilo la Ngao ya Jamii,litakalopigwa Uwanja wa Taifa,Dar  Es Salaam,litakuwa hitimisho la tambo za mashabiki wao,huku wale wa Simba wakionekana kuwanyong’onyesha wenzao wakitambia usajili wao wanaodai umewapatia kikosi bora na kipana zaidi.

Ally Yusuf “ Tigana” winga wa zamani aliyepata kuzichezea timu hizo kwa nyakati tofauti,amenukuliwa na vyombo vya habari,akisema mchezo huo si mwepesi kutokana na tabia za Klabu hizo,kwa kuwapa ujiko ama kuwatibulia makocha ,viongozi na wachezaji.

Mdau Mkubwa wa Soka Nchini na Mwalimu wa Soka,Imam Mabrouky,anasema pamoja na changamoto zinazotokea kwa pambano la Watani wa Jadi,lakini kuna haja ya kuzama zaidi katika kubadili mifumo ya timu hizo ambazo ndio dira ya soka la nchini,hatua itakayosaidia kupata maendeleo ya mchezo wa soka.

Nae Zamoyoni Mogella “Golden Boy”,mshambuliaji mahiri wa zamani wa timu hizo na Taifa Stars,amesema mchezo wa watani wa jadi daima huwa haitabiriki,bali timu yenye nidhamu ndio huibuka mshindi.

Ama hakika pambano la timu hizo si rahisi kumtabiri mshindi,kwani mara nyingi huwa na matokeo ya kushangaza,kwani huwa zaidi ya kuwa na kikosi bora kwa wakati huo,uchumi mzuri uliosaidia usajili na maandalizi mazuri lakini matokeo yakawa hasi.

Lakini hayo ni tisa,kumi ni mikasa inayoibuka baada ya pambano la Watani wa Jadi,kwani ada kutimua benchi la ufundi kwa timu inayofungwa,na pindi likisalimika basi jumba bovu hilo huwaangukia baadhi ya wachezaji hata viongozi wakidaiwa kuhujumu timu.

Katika suala la kutimua benchi la Ufundi ndilo hupewa kipaumbele na viongozi wa timu hizo kwa dhana ya kujisafisha kwa mashabiki wao na kumbukumbu zinaonesha Yanga imepata kutimua benchi lake lote la Ufundi,lililokuwa chini ya Ernie Brandts na Fred Felix “Minziro”.

Hii baada ya matokeo ya pambano la 13 Desemba 2013,la Nani Mtani Jembe,lililopigwa Uwanja wa Taifa na Wanajangwani kuambulia kichapo cha bao 3 – 1.

Pia katika  pambano hilo lilichezwa 13 Desemba 2014,halikuliacha salama Benchi la Ufundi la timu hiyo,lililokuwa likiongozwa na Kocha Marcio Maximo baada ya kupokea kipigo cha bao 2 – 0 kutoka kwa Watani zao hao,katika pambano lililopigwa pia Uwanja wa Taifa.

Simba Sports Club nao kwa nyakati mbalimbali imepata kuwatimua Milovan Circovic,Patrick Liewig,Patrick Phiri,Abdallah Kibadeni,Zdravko Logarusic,Goran Kopunovic na Dylan Kerr.

Ni utamaduni ambao hauna afya kwa soka letu nchini,lakini ndio imezoeleka kwa Klabu hizo mbili kukubali kushindwa kwa stahili hiyo ya kuwatupia lawama wachezaji kucheza chini ya kiwango,ama miongoni mwa viongozi kuhujumu mechi na kubwa zaidi ni kufukuza makocha kila kukicha.

Sasa katika pambano la leo,ni kiongozi ama viongozi pia wachezaji watakaoangukiwa na jumba bovu hilo?Na benchi lipi la Ufundi litafumuliwa?Ni kocha Joseph Omog wa Simba?ama George Lwandamina wa Yanga?Ama safari hii timu hizi zitabadilika kwa kuona vitendo hivyo vimepitwa na wakati?Muda utaamua.





KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI