B
|
unge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania limepitisha
sheria mpya ya madini,ambayo itatambua haki na
dhamana ya serikali katika
makinikia,ambayo sasa hayataruhusiwa kuchenjuliwa nje ya nchi.
Pia serikali itashiriki kwa asilimia kuanzia 16 hadi 50
katika shughuli zote za uchimbaji, uchakataji na uchejuaji madini na ununuzi wa
hisa katika kampuni ya uchimbaji madini.
Aidha,
Wakala wa Ukaguzi wa Madini (TMAA) umefutwa rasmi na sasa kunaanzishwa
Kamisheni ya Madini, na kwamba kuanzia sasa umiliki wa leseni mbalimbali
zinazotolewa kwa mujibu wa Sheria ya Madini, hautahamishwa kabla haujafanyiwa
uendelezaji katika kitalu husika.
Akielezea
mapendekezo ya Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka
2017 katika Sheria ya Madini ya Mwaka 2010, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa
Palamagamba Kabudi alisema asilimia hizo za hisa ni kwa kuangalia thamani ya
gharama ambazo serikali inahamia katika vituo vya uwekezaji na kodi aliyopewa
mwekezaji.
Profesa
Kabudi alisema muswada huo pia unatambua haki na dhamana ya serikali juu ya
makinikia na kuweka utaratibu wa kuyahifadhi sehemu maalumu migodini chini ya
uangalizi wa serikali.
“Kupitia marekebisho hayo, makinikia yanayotolewa
nchini bila kufanyiwa uchunguzi wa kupata thamani halisi kabla ya kuchenjuliwa
na uchenjuaji utafanyika nchini. Kuanzia sasa makinikia hayatauzwa nje ya nchi,
yatauzwa kwenda kwa wachenjuaji wa ndani ya nchi yakiwa ni bidhaa ambayo
itatozwa kodi,” alifafanua.
Alisema
pia muswada unaipa serikali haki na dhamana juu ya usimamizi wa bidhaa zote na
maliasili, zinazotokana na uchimbaji, uchakataji na uchejuaji wa madini
yakiwamo makinikia au kwa jina maarufu mchanga wa dhahabu.
Aidha,
alisema muswada umelenga kutambua na kuweka chini ya uangalizi wa serikali
maeneo yote ya uchimbaji na madini kwa lengo la kuweka ulinzi na usimamizi
madhubuti wa madini kwa lengo la kuweka ulinzi na usimamizi madhubuti wa maeneo
ya uchimbaji.
“Hii itasaidia kuwepo ulinzimahsusi wa maeneo yote ya uchimbaji wa
madini, kuwepo kwa utaratibu wa serikali kufanya ukaguzi na udhibiti wa
usambazaji wa madini, kuipa serikali uwezo wa kudhibiti na kutambua viwango vya
madini yote yanayotolewa kwenye maeneo ya migodi na kupitia vyombo vya ulinzi
na usalama vya serikali,” alieleza.
TMAA
yazikwa rasmi
Alieleza
kuwa kufutwa kwa TMAA kunatokana na majukumu yake, yaliyokuwa yakitekelezwa na
wakala huyo kuhamishiwa kwa Kamisheni ya Madini ambayo itaanzishwa.
Akiwasilisha
muswada huo, Profesa Kabudi alisema kutokana na kufanyiwa mapitio ya madaraka
ya Waziri na Kamishna wa Madini kwa lengo la kuwapunguza baadhi ya majukumu na
madaraka yatahamishiwa kwa Kamisheni ya Madini.
Alisema
kamisheni inayopendekezwa kuanzishwa itakuwa na jumla ya makamishina tisa, na
watu kati yao akiwamo Mwenyekiti watakuwa wa kudumu.
Alifafanua,“Watashirikiana na watendaji wakuu
kutekeleza majukumu yao ya Kamisheni ya kila siku, makamishna wengine watakuwa
wa muda na watakutana katika vikao maalumu vya kamisheni kwa ajili ya kufanya
maamuzi ya misingi na kufuatilia utekelezaji wake.”
Aidha
aliongeza kuwa makamishina wa muda watateuliwa kutokana na nafasi zao ambao ni
Katibu Mkuu Hazina, Katibu Mkuu Tamisemi, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali,
Katibu Mkuu wa Ulinzi na Katibu Mkuu Ardhi.
“Kamisheni inayopendekezwa kuundwa itachukua
majukumu sehemu kubwa ya majukumu ya Kamishna wa Madini kwa sasa. Majukumu hayo
ni pamoja na kutoa, kuhuisha au pale itakapolazimika kufuta leseni zote
zinazotolewa kwa mujibu wa sheria ya madini, kusimamia shughuli za madini ikiwa
ni pamoja na kufanya ukaguzi maeneo ya migodi.
"Pia majukumu yote yaliyokuwa yakitekelezwa na
TMAA yatahamishiwa na kuwekwa chini ya Kamishna. Na kwa msingi huu TMAA
inafutwa,”alibainisha.
Umiliki
wa leseni
Kuhusu
kutohamisha leseni, alisema hatua hiyo ni katika kuzuia watu kufanya biashara
ya udalali wa leseni.
Ameeleza,“Katika kuweka masharti yanayokusudia
kuzuia watu kufanya biashara ya udalali wa leseni mbalimbali zinazotolewa kwa
mujibu wa sheria ya madini, mmiliki wa leseni hataruhusiwa kuhamisha umiliki wa
leseni kabla ya uendelezaji katka kitalu husika.”
Aliongeza, “baada ya kumalizika kwa muda wake, leseni
itahuishwa kwa kipindi kimoja tu, na baada ya hapo umiliki wa kitalu husika
utarejeshwa serikalini.”