
Ali Yanga amefariki dunia jana tarehe 20 Juni, 2017 kwa ajali ya gari
iliyotokea katika Kijiji cha Chipogolo kilichopo katika Wilaya ya
Mpwapwa Mkoani Dodoma.
Mhe. Rais Magufuli atamkumbuka Ali Yanga kwa uzalendo wake na mchango
wake wa kuhamasisha na kushabikia masuala mbalimbali ya kitaifa na hasa
michezo, ikiwemo kuishabikia timu yake ya Yanga, timu ya soka ya Taifa,
Chama Cha Mapinduzi (CCM) na shughuli za kiserikali kama vile Mwenge wa Uhuru na ziara za viongozi.
“Nimeguswa sana na kifo cha Ali Yanga, nilikuwa nae
wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ambapo alitoa mchango
mkubwa katika uhamasishaji wa wananchi kukipigia kura chama changu cha
CCM, na pia amekuwa akiongoza mashabiki wenzake kuishabikia timu ya
Yanga na timu ya Taifa bila kuchoka. Kwa kweli alikuwa hodari sana
katika ushabiki wake.
“Natoa pole nyingi sana kwa familia yake, viongozi wa
timu ya Yanga, wanamichezo wote, wana CCM na wote walioguswa na kifo cha
Ali Yanga na namuombea kwa Mwenyezi Mungu aipumzishe roho yake mahali
pema peponi, Amina” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kibaha, Pwani.
21 Juni, 2017