IMEFAHAMIKA kwamba pamoja na mkoa wa Shinyanga
kuwa ni miongoni mwa mikoa nchini inayopata mazao mengi ya chakula kila msimu
wa kilimo,huku jamii yake ikionekana na maumbo makubwa,lakini inakabiliwa na
tatizo la upungufu wa damu kwa watoto.
Tatizo hilo ambalo limekuwa
sababu ya kuwepo kwa vijana wengi waliodumaa,limeelezwa kutokea kwa watoto
wengi mkoani humo kutokana na jamii yake kutozingatia lishe bora kwa wakazi
wake imesababisha tatizo la udumavu na upungufu wa damu kwa watoto,mkoani humo.
Mganga mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga, Dr. Ntuli Kaporogwe,ameyabainisha hayo kwenye mdahalo uliohusu
matumizi ya chakula na lishe, ambapo alisema licha ya wakazi mkoani humo
kuonekana na maumbo makubwa,lakini
asilimia 71 ya watoto wanamatatizo ya upungufu wa damu.
Dr. Kaporogwe alisema tatizo
hilo la damu linachangia udumavu wa afya
kutokana na wazazi wengi kutozingatia matumizi ya chakula chenye lishe pamoja
na kuwa na chakula cha kutosha lakini hakitumiwi kwa kuzingatia matumizi halisi
ya chakula kwa binadamu.
Alisema sababu nyingine
inayochangia kuwepo kwa tatizo hilo ni kutokana na jamii hiyo kukabiliwa na changamoto kubwa juu ya uelewa wa matumizi
ya vyakula vyenye madhara mwilini,ambapo asilimia 70 ya chumvi inayouzwa Mkoani
Shinyanga haina madini joto, hali ambayo inaleta madhara kwenye ubongo wa
binadamu kuanzia akiwa mtoto mdogo.
Akizungumza katika mdahalo
huo; Afisa lishe Mkoa wa Shinyanga, Mariam Mwita,alisema tatizo la udumavu kwa
watoto chanzo chake kinaanzia kwa mama mjamzito,kutozingatia lishe wakati wa
ujauzito hali ambayo inachangia kuzaliwa mtoto akiwa na hali hiyo.
Mwita alisema tatizo hilo
limekuwa likichangiwa na mfumo dume uliojengeka kwenye jamii kwamba mwanaume
ndio mwenye mamlaka ya kupanga lishe bila kumsikiliza mwanamke anapokuwa
anaeleza hali ambayo inachangia tatizo kuwepo kubwa mkoani Shinyanga tofauti na
mikoa mingine ya hapa nchini
Aidha Mwita alisema pamoja
na kuwepo idadi kubwa ya watoto wenye upungufu wa damu pia kuna tatizo kubwa la
utapiamlo na ugonjwa wa kuhara kwa watoto hali ambayo alipendekeza Halmashauri
zote Mkoani Shinyanga kuwa na mikakati wa kushirikisha idara zote zinazohusika
na chakula kukabiliana na tatizo la lishe
Nae Mratibu wa Mpango huo
wa chakula na lishe, kutoka Shirika la HUHESO FOUNDATION, Juma Mwesigwa,alisema
mpango mkakati wa kupambana na tatizo la lishe Tanzania unatekelezwa na zaidi
ya mashirika mia tatu chini ya mwamvuli wa shirika mama la PANITA.
Mwesigwa ambaye pia ni
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la HUHESO FOUNDATION alisema katika kanda
ya Ziwa Magharibi,inayojumuisha mikoa mitatu ya Shinyanga,Kagera na Geita kuna
jumla ya mashirika manane mwanachama wa shirika mama la PANITA,yanayojishughulisha
na mapambano ya kuondoa tatizo hilo.