Monday, July 11, 2016

WANUNUZI WA PAMBA,BODI WATUNISHIANA MISULI BEI ELEKEZI.

BOFYA HAPA CHINI KUONA MAAJABU YA LEO



WAKATI serikali kupitia Bodi ya Pamba Tanzania ikiweka msimamo wa kuhakikiasha wanunuzi wa zao hilo kununua kwa bei elekezi ya Shiiliingi Elfu Moja kwa kilo,wamiliki wa Makampuni hayo ya kununua kupitia chama chao wamegoma wakidai wanunue kwa Shilingi Mia Nane kwa kilo moja.

Mvutano huo wa Bei umesababisha baadhi ya wakulima kuuza pamba hiyo kwa Walanguzi kwa bei ya Sh 700/-(Mia saba )kwa kilo moja,baada ya makampuni hayo kugoma kununua zao hilo tangu msimu ufunguliwe Juni 26,mwaka huu,na serikali kutangaza bei hiyo elekezi kwa kilo moja.

Hata hivyo wakati mvutano huo ukiendelea kuwaumiza Wakulima kwa pamba yao kununuliwa na walanguzi licha ya bei ya chini ,mizani wanazotumia hazijathibitishwa na Wakala wa Vipimo Tanzania,hali ambayo inachangia kupunjwa kwa kilo.Waziri wa Kilimo,Mifugo na Uvuvi;Charles Tizeba,alisema suala hilo linashughulikiwa kiofisi.

Tizeba alisema kwa sasa wanaopaswa kuzungumzia ni Bodi ya Pamba Tanzania,kwakuwa ndio wasimamizi na wadhibiti wa zao hilo ingawa alisema Wizara kama Wizara inalishughulikia kiwizara,kuona hali itakavyokuwa katika kuwasaidia Wakulima na wanunuzi.

Kabla ya hapo Katibu wa Chama cha Wanunuzi wa Pamba Tanzania,Boaz Ogola,alisema bei hiyo ya 1000 kwa kilo iliyotolewa na serikali ni kubwa ikilinganishwa na kushuka kwa bei ya soko la Dunia pamoja na kuporomoka kwa thamani ya Shilingi.

Ogola alisema mpaka sasa wanunuzi wote wamegoma kukunua zao hilo kutokana na hali halisi ya bei hiyo kuonyesha hasara moja kwa moja hasa kwakuwa pamoja na kununua bei hiyo bado kuna kodi mbalimbali za serikali pamoja na ushuru katika Halmashauri hali ambayo tayari wameandika barua kuelezea hali hiyo kwa Waziri Mkuu.

Kufuatia hali hiyo kwa sababu bei ya kununulia na kuuzia iko wazi kwenye mtandao,Ogolo alisema baadhi ya benki zimegoma kuwapa fedha wanunuzi hao kwa kuhofia kupoteza fedha zao kwa makampuni hayo ya Wanunuzi wa Pamba kupata hasara kutokana na kushuka kwa zao hilo kwenye soko la dunia.  

Pamoja na maelezo hayo ya wanunuzi wa zao hilo,Bodi ya Pamba Tanzania kupitia Mkurugenzi wake Gabriel Mwalo,wamesema hawana mpango wa kupunguza bei hadi kufikia Shilingi Mia Nane kwa kilo,kama vile wanunuzi wanavyotaka.

Mwalo alisema wanunuzi hao wameandika barua ya kuomba kupunguziwa bei kwa Waziri Mkuu,lakini ombi ni ombi tu ambalo linaweza kukubaliwa ama kukataliwa na kuongeza kuwa Serikali haina mpango wa kupunguza Bei hiyo kwakuwa lengo lake ni kuhakikisha wakulima wa Pamba wananufaika  na kilimo hicho.

“Hao wanunuzi wako likizo tu,wanategeana kununua wakiona wenzao wananunua na wao watanunua tu,kwakuwa maombi yao ya kupunguziwa bei kwa waziri mkuu mpaka sasa zaidi ya wiki tangu wapeleke hakuna majibu hivyo sisi kama Bodi hatuwezi kuzungumzia punguzo la bei tunachozungumzia ni bei ya Elfu Moja iliyopo kwakuwa hakuna maelekezo mengine ya Serikali kuhusu bei elekezi,”alisema Mwalo.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama cha Wakulima wa Pamba Tanzania,George Mpanduji,aliomba Serikali kama kweli lengo lake ni kuwasaidia Wakulima wa Pamba,lazima iangalie pande zote mbili,wanunuzi na wakulima kwa kufuta ama kupunguza baadhi ya kodi na ushuru kwenye zao hilo.

Mpanduji alisema wakulima kwa sasa wameipokea vizuri bei ya Elfu Moja kwa kilo ili waweze kunufaika nayo,lazima Serikali ilegeze masharti kwa wanunuzi ili iwawezeshe kununua bila hasara kuliko ilivyo sasa Kodi na Ushuru ni mwingi hali iliyosababisha wanunuzi hao kugoma kununua wakiogopa hasara.

Kugoma kwa wanunuzi hao,Mpanduji alisema kumesababisha kuvamiwa na walanguzi vijijini ambao wanawanunulia pamba hiyo kwa bei ya Shilingi Mia Saba,kwa kilo bada ya Mia Nane  ya wanunuzi na Elfu moja ya Serikali na wanawanunulia kwa kutumia mizani zilizochakachuliwa ambazo zinawaibia wakulima hao ambao wengi wao wanamahitaji ya kupata fedha ambazo hawazipati kutokana na makampuni hayo kugoma kununua

KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI