JESHI
la Polisi mkoani Dodoma linawashikilia viongozi watatu wa Baraza la
Vijana la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bavicha) Taifa,akiwemo Mwenyekiti Bavicha Taifa,Patrobas Katambi,kwa
uchochezi na kuikashifu serikali.
Pia viongozi hao wanadaiwa kuvaa fulana zenye maandishi demokrasia imenyongwa, huku nyingine zikiandikwa dikteta uchwara.
Wanaoshikiliwa pamoja na Mwenyekiti wa Bavicha- Taifa, Katambi,ni Katibu wa
Bavicha-Taifa, Julius Mwita na Mwenyekiti wa Bavicha mkoani Mbeya,
George Tito.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema watuhumiwa hao
watashikiliwa mpaka Jumatatu watakapofikishwa mahakamani.
“Hawatadhaminiwa mpaka Jumatatu, watakapofikishwa mahakamani,” alisema.
Kamanda
Mambosasa alisema kitendo cha viongozi hao kuvaa fulana inayosema
demokrasia imenyongwa, inamaanisha serikali inanyonga demokrasia, jambo
ambalo ni la uchochezi.
Akizungumza
na waandishi wa habari kuelezea tukio hilo Mjumbe wa Baraza Kuu la
Chadema-Taifa, Joseph Kasambala alidai walikuwa katika ziara katika
baadhi ya mikoa, wakianzia mkoani Mara katika Kijiji cha Mwitongo,
Mwanza kabla hawajafika Dodoma juzi saa 8:00 mchana.
Alisema
jana walikusudia kukutana na vyombo vya habari mjini Dodoma kuelezea
hatua iliyofikiwa katika mpango wao wa Bavicha – Taifa kushirikiana na
Jeshi la Polisi mkoani Dodoma, kuzuia wanachama wa CCM kufanya Mkutano
Mkuu wa Taifa, Julai 23 mwaka huu.
Alidai
wakiwa katika baa ya Cape Town, usiku aliwaacha wenzake na kwenda
kukutana na jamaa yake mwingine na baadaye alipata taarifa za wenzake
kukamatwa na polisi.
Kwa
mujibu wa madai ya Kasambala, kilichomsikitisha ni kukataliwa kuonana
nao alipofika kwenye kituo kikuu cha polisi jana asubuhi ambapo
alitakiwa kwanza akaonane na viongozi wa Polisi wa wilaya na mkoa (OCD,
RPC).
Kasambala
alidai taarifa alizopatiwa kwenye kituo hicho cha polisi, zilieleza
kuwa kosa wanalotuhumiwa kufanya ni kukashifu serikali, kwa kuvaa fulana
yenye maandishi ‘Dikteta Uchwara’, tuhuma alizodai kuwa si za kweli.
Alionesha
fulana aliyokuwa amevaa, yenye rangi nyeusi na maandiko meupe
yanayosema, ‘Mwl. Nyerere: Demokrasia inanyongwa’ upande wa mbele ikiwa
na maandishi ‘haki na amani’.
Alidai
kuwa ziara yao inajumuisha viongozi sita wa Bavicha, akiwemo yeye,
watatu waliokamatwa ambao ni Katibu Mwenezi wa Bavicha – Taifa, Edward
Simbeye na Katibu wa Bavichamkoani Temeke, Hilda Newton.
Kasambala
alidai kuwa baada ya kikao hicho, wangerejea Dar es Salaam, ili
kukamilisha mikakati hiyo akisema ingawa wanafahamu kuwa hawana mamlaka
ya kuzuia mkutano huo wa CCM, lakini wanao wajibu wa kushirikiana na
polisi kama raia wema, kuhakikisha maagizo ya serikali yanazingatiwa.
Hivi
karibuni, viongozi wa BAVICHA wakiwa jijini Dar es Salaam, walitangaza
msimamo wao wa kuzuia mkutano huo kwa kutumia wanachama wake wapatao
4,000.
Makamu
Mwenyekiti wa Bavicha, Patrick ole Sosopi, alidai kuwa vijana hao
watatoka sehemu mbalimbali ili kuzuia mkutano huo wa CCM ili kusaidia
Jeshi la Polisi kutekeleza amri yake ya kuzuia mikutano ya kisiasa hadi
2020.
KUONA VIDEO MPYA BOFYA HAPA CHINI