MAMLAKA ya Mawasiliano
Tanzania(TCRA),imewaonya wauzaji wa
vifaa vya mawasiliano ya mkononi(simu)kuacha kufanya hila ya kubadilisha namba
tambulishi ya vifaa hivyo(mobile devices)kwa
lengo la kupata wateja kipindi hiki cha kuelekea kuzimwa kwa simu bandia.
Onyo hilo lilitolewa na
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA,Mhandisi James Kilaba,wakati akitoa
tathimini ya hali halisi kuelekea ukomo
wa matumizi ya simu bandia nchini,Juni 16,mwaka huu,kwa kubainisha ni kosa
kisheria kwa wauzaji wa simu kubadilisha namba hizo.
Mhandisi Kilaba alisema
kumekuwepo hila zinazofanywa na wauzaji wa simu,kubadilisha namba tambulishi
ambazo kufikia Juni 16,mwaka huu simu hazitafanya kazi,kwa kuweka namba za
hadaa kusudi wafaulu kuuza simu hizo,jambo ambalo ni kosa kisheria.
Hivyo alitoa onyo kwa
wauzaji watakaobainika kubadilisha namba hizo,watachukuliwa hatua za kisheria
ikiwa ni pamoja na kulipa faini ya Sh.Milioni 30 au kifungo kisichozidi miaka
kumi.
Hata hivyo aliwakumbusha
wateja pindi wanaponunua simu wanapaswa kuhakiki ili kubaini kama hazitokuwa na
matatizo baada ya mwezi Juni,hasa baada ya kubaini kuwepo kwa vitendo vya hila
vinavyofanywa na wauzaji kwa kuingiza
namba mpaya kusudi wafanikiwe kuuza simu zao.
“Wateja wanapaswa kuwa makini
kipindi hiki kuelekea Juni 16,mwaka huu,kwani kumekuwepo hila kwa baadhi ya
wauzaji simu kuingiza namba mpya kusudi wafanye biashara,lakini watambue hizo
ni hila zitakazojenga chuki,kwani muda ukifika hazitafanya kazi,”alisema
Mhandisi Kilabo.
Aliwasihi wauzaji hao
kuhakikisha wanakuwa waaminifu katika ya biashara ya simu,ikiwa ni pamoja na
kuepuka kutoa bei za punguzo za simu za simu huku wakitambua simu hizo ni
bandia.
Alisema tangu Desemba
mwaka jana hadi kufikia April mwaka huu,TCRA imetoa elimu juu ya kuhakiki simu
katika mikoa kumi nchini,huku ikijiandaa kufanya zoezi hilo katika mikoa
mingine kumi.
Ameitaja mikoa ambayo
wanataraji kutoa elimu hiyo kati ya mwezi Mei na Juni,kuwa ni Kagera,Lindi,Morogoro,Shinyanga,Pwani,Mtwara,Geita,Mara,Simiyu
na Mwanza.
Alisema kutokana na
uchambuzi wa namba tambulishi (IMEI)uliofanyika Machi mwaka huu imebainika kuwa
idadi ya namba tambulishi ambazo hazina viwango zilikuwa asilimia 13 tofauti na
Februari mwaka huu ambapo ilikuwa asilimia 18.