WAKAZI wa Kata ya
Isaka,katika Halmashauri ya Msalala,wilayani Kahama,wameazimia kuchanga zaidi
ya Shilingi 216 Milioni,kwa ajili ya kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya
Kata,utakaotatua changamoto zinazoikabili Kata hiyo katika sekta ya Afya na
Elimu.
Akizungumza katika Mkutano
wa Hadhara,Diwani wa Kata ya Isaka,Dk.Gerald Mwanzia,aliwahamasisha wananchi
kuona umuhimu wa kuchanga fedha hizo kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za
Serikali ya awamu ya tano katika kuleta maendeleo.
Dk.Mwanzia alisema pamoja
na mikakati mizuri ya Serikali katika kuhakikisha nchi inapiga hatua katika
maendeleo,ni budi wananchi kutobweteka kwa kujitoa kuchangia na kuchangia nguvu
zao hatua itakayowezesha kupiga hatua kubwa ya maendeleo.
“Tuna changamoto kubwa
katika Kata yetu,lakini ni vyema tuweke vipaumbele vya elimu na afya,tujitoe
kwa moyo mmoja kuchanga kwa hiari fedha ili kuboresha miundo mbinu katika sekta
hizo,ndipo tuipigie kelele serikali kuu kutuongezea nguvu,”alisema Dk.Mwanzia.
Alisema kutokana na Kata hiyo kukabiliwa na changamoto
za Afya na Elimu,Kamati ya Maendeleo ya Kata ilifanya utafiti kisha kuafikiana
ni budi kutengeneza mpango mkakati wa maendeleo ambao ni kuanzisha Mfuko huo ili
kukabiliana na tatizo hilo,kwa kupendekeza kila mtu mwenye uwezo wa kufanya kazi
achange kiasi cha Shilingi Elfu 36 kwa miaka mitatu.
Aidha alisema Kata hiyo
ambayo ina wakazi 6000 wenye uwezo wa kufanya kazi,kila mmoja atawajibika
kuchanga Shilingi Elfu 12 kwa mwaka,huku ukiandaliwa mpango madhubuti wa
kuwafikia wadau wa maendeleo waliopo katika Kata hiyo kama makampuni na mashirika ili
kutunisha mfuko huo.
Alifafanua Mfuko huo utasaidia kuboresha miundo mbinu ya Shule za Msingi na Sekondari,na kutengeneza mazingira bora ya kujifunzia kwa wanafunzi na kufundishia kwa walimu hivyo kuleta chachu ya ufaulu mzuri kwa vijana, sambamba na kuboresha Kituo cha Afya na zahanati ili kuleta ufanisi bora wa huduma hiyo.
Wanachi waliojitokea
katika mikutano hiyo ya kuhamasisha uanzishwaji wa Mfuko huo wa
maendeleo,walipongeza mpango huo kwa kuwa unagharama nafuu kwa mwananchi,hivyo
hawaoni sababu ya jamii kutochangia mkakati huo.
“Ningeomba tuupokee mpango
huu wa Diwani na Kamati yake ya Maendeleo ya Kata,kwa mustakabari wa sekta za
elimu na Afya,tutambue kila mtu anapenda raha,pindi vijana wetu wakifanya vyema
katika masomo ni faraja kwetu na hili linawezekana pindi miundo mbinu
ikiboreshwa,”alisema Salum Kulindwa.
Katika sekta ya Elimu Kata
ya Isaka inakabiliwa na upungufu wa madarasa 37,madawati 321 na matundu ya vyoo
105 kwa shule za msingi huku zikiwa hazina ofisi wala maktaba,huku mfuko huo
ukiwa na lengo la kuondoa changamoto hiyo kwa kipindi cha miaka mitatu sambamba
na kuipandisha hadhi Kituo chao cha Afya huku Sekondari yao wakitaka iwe na
Kidato cha tano na sita.