LIGI Kuu Tanzania
Bara(VPL)inaendelea leo kwa kukamilisha michezo miwili ya viporo;Yanga ambao ni
Mabingwa watetezi,watakuwa wenyeji wa maafande wa JKT Mgambo,kutoka
Kabuku,Handeni Tanga,mchezo utakaochezwa uwanja wa Taifa Jijini Dar Es Salaam
huku Azam FC wakiwakalibisha Majimaji ya Songea katika uwanja wao wa Chamanzi.
Yanga watashuka dimbani
huku wakiwa na kumbukumbu ya kutoshana ubavu na maafande hao katika mchezo wa
raundi ya kwanza,uliochezwa uwanja wa Mkwakani Tanga.
Kocha Msaidizi wa
Yanga,Juma Mwambusi,anasema kikosi chake kipo vizuri na wanatarajia watapata
matokeo mazuri,huku Kocha wa JKT Mgambo,Joseph Lazaro,akijinasibu kufuata
pointi tatu katika mchezo huo.
Katika mchezo utakaopigwa
Uwanja wa Chamanzi,Kocha msaidizi wa Azam FC,Dennis Kitambi,amesema
wanachohitaji ni ushindi ili waendelee kuwepo katika mbio za Ubingwa wa
VPL,huku Kocha wa Majimaji akisema anaamini kutokana na maandalizi walioyafanya
wataibuka na ushindi.
Yanga inaongoza ligi hiyo
ikiwa na pointi 59,mechi 24,ikifuatiwa na watani zake wenye uchu wa Ubingwa
baada ya kuukosa kwa kipindi cha miaka mitatu,Simba SC,yenye pointi 57,mechi
25,huku Azam FC ikiwa na pointi 55,mechi 24,hivyo ushindi wa Yanga leo
utawasogeza karibu katika kutwaa taji na
kulitetea kwa mwaka wa pili mfululizo.